*Asema zaidi ya wakulima wadogo 527,000 katika Mikoa 13 wamenufaika
WAZIRIMKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 56.45 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kilimo katika mikoa 13 hapa nchini.
Amesema mikopo hiyo imetolewa katika kipindi cha kuanzia Agosti 2015 hadi Septemba 2018, kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 3, 2018) kwenye maadhimisho
ya miaka 25 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mjini
Mororogo.
Mikopo
hiyo imewanufaisha wakulima wadogo zaidi ya 527,000 waliopo kwenye
mnyororo wa thamani wa mazao ya kahawa, karafuu, mahindi, mbogamboga na
mazao mengine.
Amesema
Serikali inatekeleza mipango mbalimbali kwa lengo la kutatua kero
zinazowakabili na kuwawezesha wakulima wadogo kujikwamua kiuchumi
kupitia kilimo.
Amesema
Juni 14, mwaka huu Rais Dkt. John Magufuli, alizindua Awamu ya Pili ya
Programu ya Kuendeleza Kilimo hapa nchini (ASDP II) yenye lengo la
kuboresha sekta ya kilimo.
Waziri
Mkuu amesema ASDP II inalenga kuhakikisha sekta ya kilimo inapewa
kipaumbele stahiki ili iweze kuleta tija kwa wakulima wenyewe na Taifa
kwa ujumla.
“Serikali
imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo
ikiwemo kutoa mikopo kwa wakulima wadogo; kuondoa baadhi ya tozo zenye
kufifisha uzalishaji.”
Pia
kuweka mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi na kutafuta masoko
pamoja na kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo ili kumuongezea tija
mkulima.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ameongeza kuwa mchango wa wakulima wadogo umewezesha Taifa
kujitosheleza kwa chakula na hata kuuza nje ya nchi mazao ya kilimo.
Hivyo,
Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi na watendaji wa Serikali kujenga
utamaduni wa kuhudhuria wa kukutana na kuzungumza na wakulima kuhusu
mahitaji hayo.
“Tunafahamu
kwamba wakulima mna changamoto nyingi zikiwemo za kisera, kirasilimali
na kiutendaji kwenye masuala ya ardhi, masoko, mitaji na hata kero za
tozo na ushuru.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ameagiza Wakala wa Vipimo nchini (WMA) waendesha msako
utakaowanasa wafanyabiashara wanaowaibia wakulima kwa njia ya
udanganyifu wa kutumia vipimo visivyo sahihi.
Waziri
Mkuu amesema mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuwaibia
wakulima kwa kutumia vipimo visivyo rasmi achukuliwe hatua za
kisheria.
“Utaratibu wa kutumia vipimo visivyo rasmi ambavyo vimepewa majina ya lumbesa, kangomba, umejileta mwenyewe na mengine mengi lazima ukomeshwe.”
Waziri
Mkuu ameuagiza uongozi wa WMA kwa kushirikiana na halmashauri zote
nchini wahakikishe mazao ya wakulima yanauzwa kwa kutumia vipimo rasmi
ili wasiendelee kupunjwa.
Akizungumzia
kuhusu kero ya ardhi, Waziri Mkuu amesema Serikali itawapa
wananchi ardhi inayotwaliwa kutoka kwa wawekezaji au wamiliki
walioshidwa kukidhi masharti na yale yasiyoendelezwa kwa muda mrefu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
JUMATANO, OKTOBA 3, 2018.
No comments:
Post a Comment