Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata
26 za Tanzania Bara.
Majimbo
hayo ni pamoja na Jimbo la Babati Mjini lililopo Halmashauri ya Mji wa Babati
Mkoani Manyara na Jimbo la Ukerewe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkoani
Mwanza
Akisoma
taarifa kwa umma Jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi) Makamu Mwenyekiti wa NEC,
Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salum Mbarouk amesema kwamba uchaguzi huo
utafanyika sambamba na uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro na Serengeti pamoja na
kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa awali.
“Nafasi
hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa Majimbo hayo Bwana. Joseph Michael
Mkundi (Ukerewe) na Bi. Pauline Philipo Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka
kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” alisema Jaji Mbarouk.
Alifafanua
kwamba Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya
Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Majimbo hayo
mawili.
“Uchaguzi
huu mdogo katika Majimbo ya Babati Mjini na Ukerewe utafanyika sambamba na
uchaguzi katika Majimbo ya Serengeti, Simanjiro pamoja na Kata 21 zilizotangazwa
awali….,” alisema.
Akisoma
ratiba ya uchaguzi huo, Jaji Mbarouk amesema “fomu za uteuzi wa wagombea
zitatolewa kati ya tarehe 28 Oktoba hadi
3 Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu, kampeni
za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 4 Novemba hadi tarehe 1 Desemba mwaka huu na siku ya uchaguzi
itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu”.
Ametoa wito
kwa wadua wa uchaguzi “Tunapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa
uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na
maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha
Uchaguzi huu mdogo”.
Katika
hatua nyingine, Jaji Mbarouk amesema Tume imepokea taarifa kutoka kwa waziri
mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini
ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume
uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 26 za Tanzania Bara.
Aliongeza
kuwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha
37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 13(3) cha
Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatoa
taarifa kwa Umma kuhusu uwepo wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Majimbo ya
Babati Mjini na Ukerewe pamoja na Udiwani
katika Kata Ishirini na Sita (26) za Tanzania Bara.
Majina ya
Halmashauri na Kata zenye uchaguzi kwenye mabano ni kama ifuatavyo, Halmashauri
ya Wilaya ya Temeke (Mtoni), Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (Mnyamani), Halmashauri
ya Wilaya ya Kondoa (Salanka), Halmashauri ya Wilaya ya Magu (Kabila),
Halmashauri ya Misungwi (Sumbugu, Buhingo), Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe (Bukiko),
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (Miteja, Kivinje, Singino, Somanga na Mitole).
Nyingine ni
Halmashauri ya Wilaya ya Songea (Matarawe, Ruvuma), Halmashauri ya Wilaya ya
Nyasa (Mtipwili), Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (Magange, Ring’wani, Rung’abure,
Natta na Rigicha), Halmashauri ya Mji wa Babati (Maisaka), Halmashauri ya
Wilaya ya Meru (Nkoanekoli), na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti (Salale).
No comments:
Post a Comment