Na Mwandishi Wetu, Kibaha
Benki ya CRDB Bank Plc imetoa msaada wa viti na meza 34 kwa Shule ya Sekondari Mwakamo Ruvu iliyopo katika kijiji cha Minazimikinda, kata ya Ruvu, wilayani Kibaha Vijijini mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuunga mkono sekta ya elimu nchini.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Pwani, Badru Idd alisema benki hiyo imeendelea kufanya vizuri kiuchumi ambapo katika robo tatu ya mwaka huu imeongoza kwa kupata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 206, kiwango ambacho hakuna benki nyingine nchini iliyofikia.
Alisema kwa upande wa mali za benki (total assets), CRDB imefikia zaidi ya shilingi trilioni 23 huku kiwango cha amana kikifikia trilioni 16, jambo linaloonesha ukuaji mkubwa wa benki hiyo.
“Ukuaji wa uchumi unahitaji fedha hizi kuzungushwa kwa wananchi, vikundi, taasisi, makampuni na serikali. Hivyo tumeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 13 huku matawi yetu yakifikia zaidi ya 250 nchi nzima ili kuwafikia wananchi kwa urahisi,” alisema Badru.
Aliongeza kuwa benki hiyo imekuwa na utamaduni wa kutenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kurudisha kwa jamii kupitia sekta kuu tatu ambazo ni elimu, afya na majanga.
Kwa upande wa elimu, alisema CRDB imekuwa ikisaidia ujenzi wa miundombinu ya shule, madarasa pamoja na utoaji wa madawati, viti na meza katika maeneo mbalimbali nchini.
“Katika mwaka uliopita, CRDB ilitoa msaada wa madawati katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani. Hii ni sehemu ya kutekeleza malengo yetu kama benki lakini pia kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuboresha huduma za kijamii,” alisema.
Aidha, aliwataka wanafunzi wa shule hiyo kuyatunza madawati hayo ili yadumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wengine wanaokuja baadaye.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Siza Mwakajinga alisema shule hiyo ni mpya kwani ilianza mwaka 2026 na bado inahitaji vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia.
“Tunawashukuru sana CRDB kwa msaada huu. Sasa wanafunzi wetu wanakaa kwenye madawati bora ambayo yatawasaidia katika mazingira mazuri ya ujifunzaji. Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya elimu,” alisema.
Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha shule mpya zinazojengwa zinapata huduma na vifaa muhimu kwa ajili ya wanafunzi.
Kwa upande wake, uongozi wa shule hiyo ulisema msaada huo utaleta matokeo chanya kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla huku ukiishukuru CRDB kwa kuendelea kugusa maisha ya Watanzania kupitia sekta ya elimu.




No comments:
Post a Comment