HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

May 08, 2026

CRDB Bank Foundation Yatoa Bilioni 21 Kuwainua Vijana na Wanawake

TAASISI ya CRDB Bank Foundation⁠ imetoa jumla ya shilingi bilioni 21 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake pamoja na biashara changa (startups), hatua iliyosaidia biashara 701 kupata uwezeshaji na nyingine kukua hadi kuanzisha viwanda vidogo.


Taasisi hiyo pia imeanza utekelezaji wa programu ya Go Green na Imbeju iliyozinduliwa Februari 12, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ambapo takribani vijana 3,500 walituma maandiko na proposal zao kupitia mfumo wa kidijitali wa Fursa Hub kuwania nafasi ya kushiriki programu hiyo.



Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya programu hiyo jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation⁠, Tully Esther Mwambapa amesema vijana 456 walioomba wamechaguliwa na kamati maalumu iliyoundwa na wataalamu kutoka serikalini pamoja na taasisi hiyo baada ya mapendekezo yao kupitiwa.



Amesema vijana hao wataanza kupata mafunzo yatakayogharamiwa na taasisi hiyo yakihusisha maeneo ya uwekezaji, kilimo, biashara na usimamizi wa fedha binafsi kupitia wataalamu mbalimbali wakiwemo kutoka SUGECO.


“Tunalenga kuhakikisha kila mshiriki anapata msaada unaolingana na mahitaji yake. Wapo watakaohitaji mitaji, wengine kuunganishwa na masoko au wawekezaji, na wengine kupewa ushauri wa kukuza biashara zao,” amesema Tully.


Aidha amesema maombi yalipokelewa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa idadi kubwa ya waombaji, ukifuatiwa na Arusha, Dodoma pamoja na Morogoro.


Kwa mujibu wa Tully, programu hiyo ni mwendelezo wa jitihada zilizoanza mwaka 2023 kupitia programu ya Imbeju pamoja na miradi mingine ikiwemo Ajira Yetu, Gen Z na Funguo inayotekelezwa kwa ushirikiano na UNDP, COSTECH pamoja na Wizara ya Vijana.


Amesema programu hizo zimeendelea kuleta mafanikio makubwa kwa vijana wengi nchini, huku baadhi ya wanufaika waliopata mafanikio wakirejea kuwafundisha vijana wenzao namna ya kukuza biashara na kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.






No comments:

Post a Comment

Pages