Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (kulia), akipata maelezo kutoka kwa Innocent Mabilika (kushoto), mwanafunzi anayesoma Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam aliyebuni trekta linaloweza kuvuna mpunga katika uzinduzi wa IMBEJU-UDSM Startup Challenge 2026, mradi unaotekelezwa kwa pamoja na CRDB Bank Foundation na chuo hicho, uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa. PICHA: JUMANNE JUMA.
Na Mwandishi Wetu, | Dar es Salaam
Fursa kwa vijana nchini zinaendelea kupanuka kwa kasi, huku serikali ikiweka mkazo zaidi katika ubunifu na matumizi ya teknolojia kama njia ya kujikwamua kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati wa uzinduzi wa programu ya IMBEJU – UDSM Startup Challenge 2026, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Vijana wenye mawazo bunifu wana nafasi kubwa zaidi sasa kuliko wakati wowote uliopita,” alisema Prof. Mkenda.
Alifafanua kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuwawezesha vijana kubadili mawazo yao kuwa miradi halisi ya kibiashara. Kupitia mashindano hayo, washiriki watapata mafunzo ya kitaalamu, ushauri wa kibiashara pamoja na mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara zao.
Mbali na hilo, Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa elimu ya vitendo, akieleza kuwa serikali inaendelea kuimarisha vyuo vya ufundi na elimu ya juu ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika sokoni.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, aliwataka vijana kutumia fursa hizo kwa uwajibikaji, uzalendo na kuzingatia maadili.
“Ni wakati wa vijana kushirikiana na kubuni suluhisho za changamoto za ajira badala ya kusubiri ajira,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alisema taasisi hiyo inalenga kuwezesha ubunifu 100 kupitia programu hiyo, hatua inayotarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 500 kwa vijana.
Aliongeza kuwa baadhi ya mawazo bunifu tayari yako hatua za mwisho za kuingia sokoni, akibainisha kuwa takribani mawazo 30 yana uwezo wa kuanza kutekelezwa mara moja.





No comments:
Post a Comment