NA ASHA BANI
MWENYEKITI wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Addo Novemba amesema Oktoba 31 mwaka huu kutafanyika mbio maalum zinazojulikana kwa jina la Wakili Marathon katika Jiji la Dodoma.
Alisema mbio hizo zina lengo la kuchagiza utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika michezo.
Amesema marathon hiyo itawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Hamza Johari pamoja na mwanariadha nguli Alphonce Simbu ambao wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa waandaaji, washiriki watatakiwa kulipia viingilio vitakavyoanzia Shilingi 40,000 hadi 100,000 kulingana na aina ya ushiriki, huku watoto nao wakitengewa Fun Marathon maalum ambapo wataandaliwa vifaa maalum vya kushiriki mbio hizo.
“Pamoja na kuwa wataalamu wa sheria na kutetea watu mahakamani, hata kwenye mbio pia tupo. Mimi binafsi nimejisajili kukimbia kilomita 21,” amesema Addo Novemba wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya marathon hiyo.
Msanii Farid Kubanda naye ameendelea kuinadi marathon hiyo akieleza kuwa ni ya kipekee kwa kuwa itaunganisha msaada wa kisheria, burudani pamoja na michezo ya riadha.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Juma Ikangaa amesema mbio hizo zitasaidia kuibua vipaji vya wanariadha mahiri nchini kama ilivyokuwa kwa mastaa wa riadha waliolitangaza taifa kimataifa.
Aidha, wanawake wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kushiriki marathon hiyo, huku waandaaji wakisisitiza kuwa mchezo wa marathon ni msingi wa michezo mingi duniani kutokana na umuhimu wa kukimbia katika maisha ya kila siku na michezo mbalimbali.






No comments:
Post a Comment