HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 30, 2018

ASILIMIA 85 YA WANAWAKE MKOANI MARA WANAJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiendelea na ziara ya ukaguzi hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya mmoja kati ya wagonjwa waliofika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Picha2.Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akitoa maoni juu ya namba za mawasiliano zilizopo kwenye ubao mdogo wa matangazo katika Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Mara, pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Watumishi wa sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara(hawapo kwenye picha) pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma katika.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akihoji juu ya gharama za huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, pindi alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma na miundombinu katika Hospitali hiyo.
Watumishi wa Kada mbali mbali za Afya wakimsikiliza mgani rasmi Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na uboreshaji wa miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
 Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Na WAMJW - MARA

Asilimia 85 ya Wanawake Mkoani Mara wanajifungua kwenye vituo vya Afya, hali iliyosaidia kupunguza idadi kubwa ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Mara kukagua hali ya utoaji Huduma.

"Mko Asilimia 85, kitaifa tupo Asilimia 51, kwahiyo niwapongeze kwa hilo, lengo letu ilikuwa ifikapo 2020 tunataka angalau Asilimia 80 ya wanawake wajawazito wajifungulie kwenye vituo vya Afya" Alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy ameitaka Mikoa mingine nchini kuiga jitihada zinazofanywa na mkoa wa Mara za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanawake wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

"Sitaielewa mikoa mingine kwa kushindwa kuhamasisha na kuweka Mazingira mazuri kwa wanawake kwenda kujifungulia katika vituo vya kutoa huduma za Afya" alisema Waziri Ummy

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kuhamasisha jamii hususan wanawake katika maeneo mbali mbali kuhudhuria kliniki angalau Mara 4 katika kipindi cha ujauzito.

"Wanawake ambao wanahudhuria Kliniki angalau mara 4 ni Asilimia 45 hivyo hamjafanya vizuri kwasababu kitaifa ni Asilimia 51, mjenge tabia ya kuwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki angalau Mara 4, kama watoa huduma za Afya wanavyotushauri" alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Francis Mwanisi Kuhakikisha ifikapo Disemba 30 mwaka huu angalau kaya zote mkoani Mara ziwe na vyoo bora, na kumtaka kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora kiafya na kiuchumi kwa mwanadamu.

"Kaya zilizo na vyoo bora kwa Mkoa wa Mara naona ni Asilimia 40, Kwahiyo tunahitaji kuongeza elimu na kutoa mwamko kwa jamii kuhusu kujenga vyoo bora na kuvitumia" alisema Waziri Ummy

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za Afya Mkoani Mara kupitia kuboresha Vituo vya Afya 14, na kujenga Hospitali 3 za Wilaya ambazo ni Lorya, Musoma DC na Bunda, jambo ambalo litalopunguza mzigo kwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kujikita katika kutoa huduma za rufaa.

Sambamba na hilo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma Bora kwa wananchi kwa kupeleka jumla ya Watumishi 25 katika Hospitali ya Mkoa wa Mara huku akiwahasa Viongozi mkoani hapo kujenga Mazingira mazuri yakuwavutia Watumishi ili wafanye kazi kwa bidii na wabaki katika vituo vya kazi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dkt. Hosea Bisanda alisema kuwa Hospitali ya Mkoa imeweza kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 23 mwaka 2015, vifo 14 mwaka 2016, vifo 10 mwaka 2017, na vifo 6 hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Dkt. Bisanda amesema kuwa licha ya Serikali kuwaletea Watumishi 25 Hospitali ya Mkoa wa Mara inatakiwa kuwa na Watumishi 684, lakini Watumishi waliopo sasa ni 305, hivyo kupelekea kuwa na upungufu wa Watumishi 379 sawa na Asilimia 55.

"Hospitali ya Mkoa wa Mara ina uhaba wa Watumishi hasa Madaktari Bingwa, Madaktari wasaidizi, Wauguzi, wateknolojia, Maabara pamoja na wateknolojia madawa" alisema Dkt. Hosea Bisanda.

No comments:

Post a Comment

Pages