Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Dkt. John Jingu akiongea na wataalamu
wa Maendeleo ya Jamii wakati wa kufunga mkutano wao wa mwaka mkoani
Arusha. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW.
Naibu
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia , Wazee, na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Wataalam
wa Maendeleo ya jamii wakati wa kufunga mkutano wao wa mwaka uliofanyika
mkoani Arusha .
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia , Wazee, na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikabidhi ngao kwa
mwakilishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Bi.Diana Mchonga baada ya
Halmashauri yake kufanya vizuri katika mikopo inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo
ya Wanawake (WDF) wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa wataalam wa Maendeleo ya
Jamii mkoani Arusha.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee, na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipokea zawadi ya mpira wa
miguu uliobuniwa na mmoja wa wajasiliamali unaotengenezwa kwa kutumia taka alipotembelea
mabanda ya maonesho mara baada ya kufunga mkutano wa mwaka wa Watalaam wa Maendeleo ya Jamii mkoani Arusha.
Na Anthony Ishengoma, Arusha
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameagiza Wataalam wa Maendeleo Nchini kuacha kufanyia kazi uani
nakuwataka kujitokeza sebuleni ili jamii ya Watanzania na Serikali waweze
kutambua kazi wanazozifanya
Amesema hayo jana wakati wa
hotuba yake ya kufunga Kongamano la kitaifa la Wataalam wa maendeleo ya jamii Nchini
lililohitimishwa Mjini Arusha kwa lengo la kubadilishana uzoefu, mbinu na
weledi ili kutekeleza majukumu ya kuhamasisha jamii kwa umahiri katika kufikia
uchumi wa kati.
Aidha Dkt. Ndugulile aliongeza
kuwa kazi ya wataalam wa maendeleo ya Jamii hazionekani hivyo anamwagiza
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara yake Bw. Patrick Golwike kuandaa
mwongozo utakaowawezesha wataalam hao kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
‘’Najua mnatumika kama kiraka
kwani katika maeneo yenu ya kazi mmekuwa mkiagizwa kufanya kila aina ya kazi
kwani utasikia wanasema kuwa kazi hii acha tumshirikishe yule Afisa Maendeleo
ya Jamii hii sisi kwetu kama Wizara lazima tuifanyie kazi’’. Alisema
Amewataka wataalam hao
kuhakikisha wanawawezesha wajasiriamali wadogo wadogo Nchini wanaazisha viwanda
vidogo vidogo na kuweka nembo za biashara yao kwa sababu bidhaa zinazotengenezwa
na wajasiriamali hao zina ubora sawa na bidhaa zinazozalishwa na baadhi ya
viwanda vikubwa.
‘’Ukitembelea na kujionea bidhaa
za wajasiriamali utagundua zina ubora sana lakini kuna changamoto ya
vifungashio kwani kuna wajasiriamali wanafunga bidhaa zao kwa kutumia chupa za maji
au makasha ya bidhaa za wazalishaji wakubwa, hivyo ni kuendelea kutangaza
bidhaa ya mzalishaji mkubwa’’. Aliongeza Naibu Waziri Ndugulile.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri Ndugulile amewaagiza wataalam
hao kushirikiana na TFDA, SIDO na TBS kuhakikisha wanatoa mafunzo ya ujasiriamali
kwa wajasaliamali wadogo ili waweze kuzalisha bidhaa bora na kuwawezesha
kuongeza thamani ya bidhaa zao kwa kutumia vifungashio vyenye ubora.
Wakati huo Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati akitoa taarifa fupi ya
mkutano huo kwa Naibu Waziri Ndugulile alisema moja ya maazimio yaliyotokana na
mkutano mkuu huo ni kuhakikisha majukumu yao wanayatafsiri kwa vitendo ili
kuiwezesha jamii ya watanzania kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Aidha, pamoja na mambo mengine
wataalam hao pia wameiomba Serikali kuongeza ajira ya wataalam hao ili waweze
kupatikana hadi ngazi ya kata kwa lengo la kuiwezesha jamii husika kutambua
fursa za kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika
maeneo yao.
Aidha Dkt. Jingu aliongeza kuwa
maadhimisho ya kikao hicho yametaka Uongozi wa Halmashauri za vijiji kutenga
maeneo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo ili kuwawezesha kufanya kazi
katika maeneo salama tofauti na sasa ambapo baadhi ya wajasiriamali hao
wanafanyia shughuli zao nyumbani mwao.
Kongamano la Wataalam wa
Maendeleo ya Jamii limefanyika sanjari na Mkutano Mkuu wa mwaka wa wataalam hao
unaoendelea mkoani Arusha na umewashirikisha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii
kutoka katika sekta ya umma, taasisi za Serikali, sekta binafsi nchini na mashirika
yasiyo ya kiserikali.
No comments:
Post a Comment