HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 29, 2018

Miaka Mitatu ya JPM, MSD Mnunuzi Mkuu wa Dawa Nchi za SADC,Hali ya Upatikanaji Dawa Yaimarika

 Mkurugenzi Mkuu wa Bahari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu, akizungumzia mafanikio ya Bohari hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano leo Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Rodney Thadeus  na kushoto ni Ofisa Uhusiano wa Bohari hiyo, Etty Kusiluka.
Mkurugenzi Mkuu wa Bahari ya Dawa (MSD), Laurean  Bwanakunu, akisisitiza kwa waandishi wa habari kuhusu mikakati ya Bohari hiyo kuendelea kuimarisha huduma zake kwa wananchi. (Picha na Frank Mvungi - MAELEZO).

Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) imefanikiwa kuchaguliwa kuwa  mnunuzi mkuu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Hayo yameelezwa leo, Jijini Dodoma katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO)  na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Rugambwa Bwanakunu alipokuwa akieleza mafanikio ya MSD miaka mitatu ya Rais Magufuli.

"Uchaguzi wa MSD kuwa mnunuzi mkuu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye unanda wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ulifanywa na Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa umoja huo. Tayari mkataba wa makubaliano kati ya MSD na sekretarieti ya SADC (MOU) umesainiwa tarehe 10 Oktoba mwaka huu," amesema Bwanakunu.

Amesema, kwa kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, kwa ajili ya nchi wanachama wa ukanda wa SADC, MSD itakuwa na majukumu makubwa matano ambayo ni, kusimamia huduma za ununuzi na usambazaji katika nchi wanachama, kusimamia takwimu na taarifa za dawa, kusimamia kanzi data (DAta base) ya bei za dawa, kutoa huduma za manunuzi za kutoa ushauri na upangaji wa bei elekezi za dawa.

Aidha amesema, hatua ya Tanzania kuwa mnunuzi mkuu wa dawa za nchi za ukanda wa SADC ni heshima kubwa kwa Tanzania kwa kuaminiwa kwa huduma bora, uwezo na kukidhi vigezo vya kitaalamu katika mnyororo wa ugavi na hivyo kutimiza Dira yake inayosema kuwa kitovu cha umahiri wa mnyororo wa ugavi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara katika bara la Afrika.

Vilevile amesema, wazalishaji wa dawa wa ndani watapata fursa ya kuuza dawa zao kwa ajili ya nchi 16 sasa, badala ya kuiuzia Tanzania peke yake.

Bwanakunu ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka mitatu kuwa ni pamoja na MSD kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, kupungua kwa bei za dawa kwa wastani wa asilimia 40, kuimarika wa hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara  katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vya Serikali na baadhi ya hospitali binafsi zilizoidhinishwa na wizara ya afya kwa wastani wa asilimia 90 na 92.

Mafanikio mengine ni kuongezeka na kuimarika kwa bajeti ya dawa kutoka shilingi Bil. 29.25 kwa mwaka wa fedha 2015/2016 mpaka Shilingi Bil. 251.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 (sawa na ongezeko la 88%), shilingi Bil. 260 mwaka wa fedha 2017/2015 na shilingi Bil. 269 mwaka huu wa fedha.

Ongezeko hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za uhaba wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hadi sasa MSD inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya 7,519 nchi nzima.

No comments:

Post a Comment

Pages