HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 18, 2018

MAWAZIRI WAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA PAMOJA YA UJENZI WA UCHUMI WA VIWANDA

Na Mwandishi Wetu
Mawaziri wa sekta za uchumi wamekutana Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa Programu ya pamoja ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda.
Akizungumza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo alisema kuwa Programu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda imejikita katika kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kuvutia sekta binafsi na kuongeza fursa za ajira.
“Programu hiyo itakuza uchumi na ujenzi wa viwanda kwa kufuata misingi na kanuni za kibiashara zinazokubalika kimataifa, ikiwakama nyenzo muhimu katika kuhakikisha viwanda vitakavyoanzishwa vinakuwa chachu ya maendeleo hapa nchini,” alisemaMhagama.
Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya dira ya Taifa ya maendeleo ya kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.
Hata hivyo, Waziri Mhagama alieleza kuwa Programu hii ya pamoja inatokana na kutegemeana kwa mipango na mikakati ya kisekta katika kufikia malengo ya Serikali kwa pamoja.
Aidha, alitoa rai kwa kila mmoja kuhakikisha sekta anayoiongoza inatoa mchango stahiki katika kufikia azma ya Serikali kwa kuweka malengo yanayotekelezeka kwa wakati na kufanya mapitio ya sera, sharia na kanuni.
“Niwaombe wote mliopo hapa kuhakikisha mnatimiza wajibu kwa kutekeleza Programu hii ya ujenzi wa uchumi wa Viwanda ikiwa njia ya uhakika katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya nchi na kuweza kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania” alisisitiza Mhagama.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahimiza Mawaziri kutekeleza yaliyopo kwenye kitabu cha mwongozo wa mazingira bora ya biashara hapa nchini “Blue Print”, ili kuendelea kuboresha zaidi masuala ya biashara na uwekezaji.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu, Prof. Faustine Kamuzora alisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiratibu program hiyo katika taasisi za Serikali kulingana na majukumu yao.
“Kila wizara iandae mpango mkakati na namna bora yakufanikisha utekelezaji wa program hiyo kwa kushauriana na wadau wa sekta binafsi ambao ni wadau muhimu”, Alisema Kamuzora.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Godfrey Mwambe alisema kuwa ni vyema kila Wizara na Taasisi zikajitathimini katika kutekeleza mikakati waliyonayo ili kuvutia wawekezaji na ujenzi wa viwanda kwenye maeneo ya msingi.
“Tunataka kuona viwanda vya hapa nchini vinakuwa ni soko la mazao yanayozalishwa moja kwa moja na wakulima” alisema Mwambe.

No comments:

Post a Comment

Pages