NA MWANDISHI WETU, LINDI
KAMPUNI ya Vodacom kupitia Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na T-MARC, wamefanya programu ya kuwaelimisha wanafunzi wa shule ya msingi Tulieni iliyopo mkoani Lindi juu ya usafi wa kimwili wakati wa hedhi (MHM), elimu ya afya ya uzazi, pamoja na kuwapatia wasichana zaidi ya 1700 waliopevuka taulo za hedhi.
Hii ni sehemu ya mradi endelevu uitwao “Hakuna wasichoweza” unaofanya kazi na Vodacom Tanzania Foundation wakishirikiana na T-MARC tangu mwaka 2012 wakilenga kuondoa vikwazo vinavyowafanya wasichana waliopevuka kushindwa kufikia malengo yao kielimu kunakosababishwa na changamoto mbalimbali wakati wa hedhi pamoja na afya ya uzazi kupitia vipindi vya mafunzo mbalimbali na ujumbe simu wa maandishi pamoja na kuwapatia taulo za kike/ sodo ambayo ni moja ya changamoto wanazo kutana nazo.
Ripoti iliyotolewa na TASAWANET mwaka 2015 inaonyesha kwamba asilimia 75 ya wasichana mashuleni wamesema kwamba hedhi inaathiri kufaulu kwao katika masomo. Pia, UNESCO imekadiria kwamba ndani ya mwaka mmoja, asilimia 20 ya wanafunzi wa kike hawahudhurii mashuleni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Jacquiline Materu alisema “Vodacom Foundation imejikita katika mipango ambayo inasaidia akinamama na watoto nchini, ili kuboresha afya zao, elimu na ujasiriamali. Tunaipongeza sana serikali kwa kufuta kodi za sodo. Sisi kama Vodacom Foundation tutaendelea kusaidia shughuli zozote ambazo zinalenga kutatua changamoto zinazowafanya wasichana washindwe kupata elimu bora”.
Hakuna wasichoweza imelenga kuboresha mahudhurio na ufaulu wa wasichana kwa kuwapatia elimu juu ya afya ya uzazi, elimu ya hedhi, jinsia, vile vile umuhimu wa kuchelewa kuanza kujihusisha na ngono. Kwa miaka sita mpango huu umewafikia wasichana zaidi ya 1000 na zaidi ya taulo za kike 10,000 ziligawiwa.
“Kupitia msaada wa Vodacom Foundation, tumeona maendeleo katika mahudhurio na ufaulu wa wasichana ambao walihudhuria mafunzo haya ukilinganisha na ambao hawajahudhuria. Wasichana hawa wana nafasi ya kufikia malengo yao na tumedhamiria kuwafikia wasichana wengi zaidi hasa hasa katika miji iliyojificha na yenye mila na fikra potofu juu ya hedhi zinazochochea changamoto hizi” alisema Hamid Al-Alawy Mratibu wa Mradi, T-MARC Tanzania.
No comments:
Post a Comment