HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 22, 2018

Tanzania kuendeleza wimbi la ushindi Tuzo za Kimataifa za DStv Eutelsat Star

Majaji wakipitia kazi za washiriki kwa umakini mkubwa.
Mwenyekiti wa jopo la majaji Dk. Khamis Kalegele (kulia) na moja ya majaji Davids Bwana ambaye alikuwa mshindi wa pili wa jumla wa tuzo hizo msimu wa sita  wakiwa katika zoezi la kupitia kazi za washiriki. 
Grace Mgaya kutoka MultiChoice Tanzania akihakiki kazi za washiriki.
 
•    Tanzania imefanya vizuri kwa misimu miwili iliyopita
    •    Feza Boys St Mary Goreti Kuiwakilisha Tanzania
    •    Maelfu ya wanafunzi kutoka
nchi zaidi ya 10 barani Africa kuchuana

Alhamis Novemba 22, 2018; Kwa mara nyingine tena Tanzania inaingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za DStv Eutelsat Star ambapo  wanafunzi Eric-Alex Khamis wa shule ya Sekondari ya Feza Boys Dar es Salaam na Priscilla Marealle wa shule ya St Mary Goreti Kilimanjaro wataipeperusha bendera ya Tanzania kwenye msimu wa nane wa tuzo hizo.

Kwa misimu miwili mfululizo, Tanzania imekuwa moja ya vinara katika tuzo hizo ambapo msimbu wa sita, mwanafunzi Davids Bwana wa Feza Boys aliibuka mshindi wa pili wa tuzo hizo kwa upande wa Insha, wakati katika msimu wa saba Taher Rashed wa Al-Madrasat-Saifiyatu- Burhaniyah ya Dar es salaam aliibuka mshindi wa kwanza upande wa uchoraji wa bango

Eric-Alex ameshika nafasi ya kwanza katika uandishi wa insha maalum na Priscilla kwa mchoro wa bango (poster) kuhusiana na sayansi ya Setelait ambapo wanafunzi zaidi ya takriban 200 kutoka shule mbalimbali nchini walishiriki katika mashindano hayo ya mwaka huu. Washindi hao walipatikana baada ya utahini uliofanywa na jopo la majaji watano wakiongozwa na Dk. Khamisi Kalegele kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Kazi za washindi hao zitawasilishwa MultiChoice Africa ambapo zitapambanishwa na kazi kama hizo kutoka kwa washindi wa nchi nyingine kote barani Afrika na hatimaye kupatikana washindi wa jumla katika kila kipengele yaani wale walioandika insha na wale walioandaa bango.

Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, amesema tuzo za mwaka huu zimekuwa na ushindani mkubwa ambapo shule kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Arusha, Dodoma, Pwani zimeshiriki. “Kuongezeka wa idadi ya wanafunzi wanaoshiriki katika tuzo hizi ni ishara njema na tunaamini kwa viwango walivyoonyesha, bila shaka msimu huu tutapata ushindi mkubwa kuliko hata ule wa msimu uliopita.” alisema Mshana.

Amesema tuzo hizi zinalenga kuwajengea vijana wetu ari ya kushiriki katika masomo ya sayansi na pia kuhamasisha ubunifu na ugunduzi katika tasnia ya sayansi. Amewataka walimu kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki katika tuzo kama hizi za kimataifa kwani ni kipimo kizuri kwa wanafunzi wetu na pia inajenga kujiamini kwa wanafunzi wetu.

Tuzo hizi ambazo zinahusisha uandishi wa insha maalum au kuandaa bango vyenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19.

Msimu huu, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango kuhusu sehemu au maeneo ambayo  setelaiti hazijatumika kwa ukamilifu katika kuharakisha maendeleo ya jamii

Kama kawaida tuzo hizi zina zawadi kabambe ambapo mshindi wa Insha atapata fursa ya kuzuru kituo cha Eutelsat nchini Ufaransa na pia kwenda Guiana kushuhudia mubashara urushwaji wa setelait angani.

Mshindi wa bango atajishindia safari ya kwenda nchini Afrika Kusini na kutembelea kituo cha anga cha nchi hiyo na pia makao makuu ya MultiChoice Africa akiwa kama mgeni maalum.  Shule zitakazotoa washindi hao zitapata zawadi ya kufungia huduma ya DStv bure.

Wanafunzi wengine waliofanya vizuri katika mchakato huo ni pamoja na Jacqueline Mbelwa Kamuzora wa Loleza Sekondari ya Mbeya ambaye ameshika nafasi ya pili kwenye insha na Julieth Massawe wa St. Mary Goreti ya Kilimanjaro aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa bango.

No comments:

Post a Comment

Pages