HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2018

Vodacom yatoa elimu ya kujikinga na Maafa Kanda ya Ziwa

NA MWANDISHI WETU, MWANZA

KAMPUNI ya Vodacom Tanzania kupitia Taasisi ya Vodacom Foundation Kwa kushirikiana na Taasisi ya Suleiman Kova Security and Disaster Management Foundation (Sukos-DMF) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya uokoaji pamoja na elimu ya namna ya kutumia vifaa hivyo kwa lengo la kukabiliana na majanga kama vile moto, mafuriko na ajali za barabarani, katika shughuli iliyofanyika kwa takribani wiki moja kwenye shule mbalimbali na fukwe zilizopo jijini Mwanza na Ukerewe.

Vifaa vilivyotolewa kama msaada kutoka Vodacom Tanzania Foundation ni makoti ya kujiokolea 1,468, vifaa vya kuzimia moto 21, mablanketi ya kuzimia moto 21, pamoja na vifaa vya kutolea huduma ya kwanza 21 ikiwa na malengo ya kusaidia shule hizi kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pindi yanapotokea.  Simu za redio 8 pamoja na suti za majini 20 ziligawiwa kwa viongozi wa fukwe za maji.

Wanafunzi zaidi ya 1,468 kutoka Shule 8 zilizopo Mwanza mjini na Ukerewe wamenufaika na msaada huo, shule hizo ni shule ya Sekondari Bwiro, Mbungo, Buguza, Irugwa, Bukiko na Bwaya zilizopo wilayani Ukerewe pia Shule za Msingi Nyamagana A na B zilizoko Jijini Mwanza. Pamoja na viongozi wa fukwe za Mkuyuni, Ihumilo, Luchelele na Sweya.

Akizungumza katika uzinduzi wa programu iliyofanyika jijini Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbo,  aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema, ‘Hivi karibuni tumekumbwa na ajali kubwa ya majini ya MV Nyerere iliyosababisha athari kubwa sana kwa jamii na Taifa kwa ujumla. 

Tunaishukuru sana taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation pamoja na SUKOS DMF kwa kusaidia shule hizi za Mwanza na Ukerewe kupata vifaa vya uokoaji na elimu juu ya namna ya kutumia vifaa hivyo ili pindi maafa kama haya yanapotokea vijana hawa wadogo wanakua na utayari wa kukabiliana na kupunguza athari zinazotokana na maafa haya’.

 Aliongeza kuwa vifaa vilivyotolewa kwa viongozi wa fukwe za ziwa Victoria vitaongeza usalama na uwezo wa kuokoa endapo majanga yatakapotokea.

Katika hafla ya kufunga shughuli hiyo iliyofanyika Viwanja vya Mongella wilayani Ukerewe, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Bi Rosalynn Mworia alisema, “Shabaha ya programu hii ni kufikia shule takribani 8 ili kutoa mafunzo ya kukabiliana na majanga ili kujiwekea utayari pindi majanga yanapotokea. Mafunzo haya ni muhimu hususani kwa ninyi wanafunzi na wakazi mliopo karibu na fukwe za Ziwa Victoria. Elimu hii itawasaidia sana wanafunzi hawa pamoja na jamii zao kujikinga na kujiokoa katika majanga mbali mbali kama lile la MV Nyerere”.

Muasisi wa taasisi ya Sukos Suleiman Kova alisema wanashirikiana na Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kuhamasisha jamii kujifunza na kujenga utayari wa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea. Aliongeza kuwa Sukos inawashukuru Vodacom Tanzania Foundation kwa kuwaunga mkono katika zoezi hilo lililoanza tangu Machi mwaka huu. Pia aliwataka wanafunzi kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika jamii pindi majanga yanapotokea.

Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Kennedy Michael Kitilusa aliishukuru Vodacom Tanzania Foundation kwa msaada wa vifaa na mafunzo yatakayowasaidia kukabiliana na majanga pindi yanapojitokeza, “Msaada huu utatusaidia kutatua changamoto mbalimbali  zilizokuwa zikijitokeza kipindi cha nyuma pale tulipopatwa na majanga, kwa mfano simu hizi zitatupa uwezo wa kutaarifiana na hivyo kuweza kufika haraka eneo la tukio ili kutoa msaada, pamoja na hayo tutaweza kuwasiliana na wenzetu walioko nchi kavu kuwajulisha kile kinachoendelea” alisema Kitilusa.

No comments:

Post a Comment

Pages