HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 28, 2018

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA SOKO LA KALANGALALA

*Azitaka halmashauri zingine nchini ziige mfano wa Mji wa Geita

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaameweka jiwe la msingi mradi ujenzi wa soko kuu la  Kalangalala katika Mji wa Geita na kuzitaka halmashauri zingine nchini kuiga.

Pia, amesema wajasiriamali waliokuwa wakifanya shughuli zao katika eneo hilo kabla ya  ujenzi watakuwa wa kwanza kupewa maeneo ya kufanyia biashara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Novemba 28, 2018) baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa soko la Mji wa Geita.

Amesema ni vema halmashauri zote zikaiga mfano wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kujenga masoko ya kisasa ili wajasiriamali wapate maeneo ya kufanyia kazi zao.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwaondolea wananchi kwa kuboresha na kuimarisha huduma za jamii.”

Hivyo, Waziri Mkuu amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel kwa kuwa mbunifu na msimamiaji mzuri wa miradi ya maendeleo.

Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji viongozi wa aina yake, ambao si wabadhilifu bali wanajali thamani na maslahi ya wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi  Gabriel ameahidi kulinda heshima ya wananchi wa mkoa huo kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa. 

Amesema atasimamia kikamilifu ujenzi wa miradi ya maendeleo, ukiwemo ujenzi wa soko la kisasa ambalo litakapokamilika wajasiriamali watafanyakazi muda wote hadi usiku.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Adolf Ritte amesema ujenzi wa mradi huo umegawanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa soko lenye majengo makubwa mawili yenye thamani ya sh. bilioni 1.9. 

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na wananchi watakaokuwa wanakwenda kununua bidhaa mbalimbali kwenye soko hilo. 

“Pia Halmashauri ya Mji nayo itanufaika kwa kuongezeka kwa mapato yake ya ndani. Ajira zitakazozalishwa sokoni hapo ni takribani 200. Faida nyingine ya mradi huu ni kumaliza mgogoro wa maeneo ya kufanyia biashara katika mji wetu.” 

Mapema leo Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Mji Geita kwenye eneo la Magogo na kisha alikwenda katika eneo la Bombambili kwa ajili ya kukagua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa ofisi za CCM mkoa wa Geita.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, NOVEMBA 28, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages