Jeshi
la Polisi nchini limetangaza kuanza kwa Operesheni kali ya kuwabaini na
kuwasaka watu wote wanaojihusisha na wizi wa mafuta katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)unaoendelea
kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Operesheni Maalum za Polisi,
Naibu Kamishna wa Polisi DCP Liberatus Sabas wakati akizungumza kwa nyakati
tofauti na wafanyakazi wanaofanya kazi katika mradi wa reli hiyo katika kambi
ya ujenzi ya Soga mkoani Pwani na
Ngerengere wakati wa ziara yake katika mradi huo kufuatia kuwepo kwa vitendo vya wizi wa
mafuta.
Sabas amesema Operesheni hiyo haitamwacha salama
yeyote atakayekutwa akishiriki na kufanikisha vitendo vya wizi katika mradi huo
na kuwataka wafanyakazi hao kuwa wa kwanza kutoa taarifa pindi waonapo viashiria
vya wizi katika maeneo yao ili mradi huo uwe salama.
“Polisi tutatumia kila aina ya nguvu zetu kuhakikisha
kuwa mradi huu unakuwa salama na tukikamata mwizi wa mafuta katika mradi huu
hatasahau maisha yake yote kwa kuwa kuhujumu mradi huu muhimu kwa taifa ni kosa
kubwa hasa ukizingatia gharama kubwa ambazo Serikali inatua kufanikisha jambo
hili” Alisema Sabas.
Katika hatua nyingine DCP Sabas amewaelekeza Makamanda
wa Polisi wa mikoa ya Pwani na Morogoro kuweka mikakati kabambe kwa
kushirikiana na Kikosi cha Polisi Reli ili kufanya doria za mara kwa mara
katika vijiji vinavyozunguka mradi huo kwa kuwa ndipo kulikobainika kuuzwa
mafuta ya wizi wa mradi huo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kikosi cha
Reli amesema wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara na wadereva wa
mitambo na magari katika mradi huo kwa lengo la kuwataka kushiriki katika kutoa
taarifa za wizi na kuacha kujihusisha na vitendo hivyo ambapo waliokamatwa
tayari wamefikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment