Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye (
wa tatu kushoto) akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamis
Kigwangalla pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakipewa maelezo na Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Godwell Meing'ataki kuhusiana na bwawa
lenye viboko wengi katika Hifadhi hiyo liitwalo Mwanambogo wakati
wajumbe ya Kamati hiyo walipofanya ziara ya kutembelea kwa ajili ya
kujionea mradi wa kukuza utalii kusini wa Regrow ulipofikia na namna
unavyotekelezwa.Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo,
Constantine Kanyasu. (Picha na Lusungu Helela)
Hatua
hiyo inakuja baada ya serikali ya Tanzania kukopa jumla shilingi
bilioni 345 kutoka Benki ya Dunia ili kukuza utalii katika maeneo ya
Kusini kupitia mradi ujulikanao kama Resilient Natural Resource
Management for Tourism Growth ( REGROW)
Hayo
yamebainishwa na Mwenyekiti Kamati hiyo, Mhe .Nape Nnauye baada ya
Kamati hiyo kufanya ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ikiwa ni
moja ya ziara ya kutembelea ukanda wa kusini kwa ajili ya kuona mkopo
huo umefikia wapi na namna mradi huo unavyotekelezwa.
Amesema
uamuzi huo wa Serikali wa kutaka kufungua Utalii wa Kusini ni wa
muhimu sana hata endapo mazungumzo hayo yanayoendelea yatakwama Serikali
ifikirie mbadala wake lengo likiwa ni kuongeza mapato yatokanayo na
utalii.
Katika mradi huo
Hifadhi za Mikumi, Ruaha, Udzungwa pamoja na Pori la Akiba la Selous
zinatarajiwa kunufaika kupitia mkopo huo lengo likiwa ni kufanya ukanda
wa kusini kuwa lango la Utalii kama ilivyo kwa ukanda wa kaskazini.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameishauri Serikali kuwa endapo fedha
za mkopo huo zitapatikana iandae utaratibu wa kuufanya mradi huo uwe wa
kibiashara badala ya ilivyo sasa ambapo kwa kiasi kikubwa matumizi ya
fedha hizo yamejikita katika uhifadhi zaidi.
Amesema
fedha inayowekezwa ni nyingi na italipwa na watanzania sasa ni vizuri
itakapowekezwa itoe matokeo yaliyokusudiwa ambayo yatafanana na thamani
ya mkopo wenyewe.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamis Kigwangalla
amesema kumekuwa na mashaka kidogo kutoka kwa Wafadhili ambao
wanatukopesha pesa hizo baada ya kuona mradi wa kufua umeme katika mto
Rufiji unatekelezwa.
Amefafanua
kuwa Wafadhili hao wanahofu kuwa kutakuwa na uharibifu mkubwa wa
mazingira na hivyo mradi wa Regrow utashindwa kutekelezwa kwa vile
kivutio katika Pori la Akiba la Selous kitabadilika sura yake
Ameelezea
kuwa Serikali imefanya jitihada za kuhakikisha kuwa mazingira ndani
ya Pori hilo hayataharibiwi na hivyo mradi wa Regrow unaweza ukaendelea
kama ilivyopangwa.
Amesema
moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali ni kuvihamisha viumbe ambavyo
vilikuwepo katika eneo linapotarajiwa bwawa kujengwa, Hivyo viumbe hao
wataendelea kuwepo na wanaweza kurudi katika eneo lao la awali.
Aidha,Mhe.Kigwangalla
amesema hata kama itatokea viumbe hao wakapotea kutokana na ujenzi wa
bwawa hilo basi viumbe na mimea iliyokuwepo katika eneo hilo
vitarudishiwa kwa sababu tayari imechukuliwa na kuhifadhiwa kwenye
maabara ya vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo hapa nchini kikiwemo Chuo
kikuu Cha Dar es Salaam pamoja na Sokoine.
"Tumewaeleza
kuwa mashaka yao hayawezi kuzuia huu mradi na bila shaka wametuelewa
hivyo tunasubilia uamuzi wa mwisho wa kuamua wanatukopesha au
hawatukopeshi" amesema Mhe. Kigwangalla.
Pia
amesema katika mradi huo yatachimbwa mabwawa makubwa matatu ambayo
yatatumika kama vyanzo vya maji kwa wanyama waliopo katika bonde la Mto
Rufiji
Akizungumzia
manufaa ya mkopo huo , Waziri Kigwangalla amesema utatumika kujenga
miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara pamoja na viwanja vya ndege
ambavyo vitakuwa vichocheo vikubwa katika kukuza na kuendekeza utalii
kwa ukanda wa kusini.
No comments:
Post a Comment