HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 13, 2019

CWT YATAKA WATENDAJI WAJALI HAKI ZA WATUMISHI

NA TIGANYA VINCENT

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya amewaomba Watendaji Wakuu wa Halmashauri ya Manispaa , Wilaya na Mji mkoani Tabora kuhakikisha wanajali haki za watumishi waliochini yao ambazo zipo ndani ya uwezo wao ili kuondoa manung’uniko yanayoepukika.

Hatua hiyo itasaidia kuendeleza mshikamano na ushirikiano baina ya watumishi na Serikali na kufanya kuwepo na utendaji wa pamoja.

Ulaya alitoa ombi hilo jana Mkoani Tabora wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani humo uliolenga kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya walimu , Serikali na CWT.

Alisema mambo mengine yanayodaiwa na watumishi wakiwemo Walimu yako ndani viongozi kama vile Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Utumishi na Maafisa Elimu wala hayaitaji viongozi wa Wizara ndio mtumishi apate haki yake.

“Nitoe ombi langu kwa viongozi wa wetu wa mkoa wa Tabora Maafisa utumishi , Maafisa Elimu na wengine wote tuhakikishe kwamba tunajali haki za watumishi wetu husasani ni walimu yapo mambo ya kawaida ambayo yapo chini yenu kama Mkurugenzi” alisema.

“Masuala kama nauli ya likizo ni nyinyi wenye huku na mambo mengine…tuendelee kuwaomba kwa sababu mshikamano huu tuhakikishe kwamba tunaendelea kutimiza wajibu wetu kwa kadiri tutakavyoweza” alisisitiza.

Aidha Ulaya alisema mwelekeo wa CWT ni kuhakikisha inasimimia wajibu wa Mwalimu kufanyakazi zake kwa ufanisi kwa sababu inaamini kuwa bila ya kutumiza wajibu walimu hawatakuwa na haki ya kudai kile wanachostahili kudai.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwataka Wakurugenzi Watendaji na wale Maofisa wanaoshughulikia masuala ya utumishi wanapowapandisha madaraja watumishi wakiwemo walimu wahakikishe wanabadilisha na mishahara yao na sio kubaki na ile ya cheo cha zamani.

Aliongeza kuwa wanawahamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine pia wanapaswa kuwalipa stahili zao kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya utumishi wa umma inavyotaka kabla hajaondoka katika kituo chake za zamani kuelekea kipya.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema kama Halmashauri zitakuwa hazina fedha katika kipindi mwalimu au mtumishi anadai ni vema wakaweka utaratibu kuwaandikia barua mtumishi la kutambua deni lake ambalo limeshaidhinishwa ofisi ya Mkaguzi wa Ndani kwamba ni halali ili hata kama ikitokea bahati mbaya akapata tatizo ndugu zake wawe na msingi wa kudai.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Tabora Hamis Lissu alisema wamekutatana kwa lengo kujenga desturi ya uwajibikaji wa pamoja katika kufikia malengo yaliyokusudiwa ya utoaji elimu bora katika Mkoa wa Tabora.

Aliongeza kuwa wamekutata ili kuondoa tofauti ndogo ndogo miongoni mwao ili kuwa na mwelekeo wa pamoja katika kuendeleza elimu kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages