HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2019

MIKAKATI RIADHA TANZANIA 2019


RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka amefanya mkutano na wadau, viongozi wa Riadha mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, sambamba na wachezaji kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya mchezo huo hasa ukizingatia mwaka huu ni mwaka wa matukio makubwa matatu ya Riadha ya Kimataifa.

Mwaka huu, kutakuwa na Mashindano ya Nyika ya Dunia- Aarhus Denmark, Mataifa ya Afrika-Casablanca Morocco na Mashindano ya Dunia-Doha Qatar.

Katika mkutano huo, Rais Mtaka akiambatana na Katibu Mkuu RT, Wilhelm Gidabuday na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, kwa pamoja waliafikiana mambo mbalimbali kuelekea matukio hayo makubwa Ki-Nchi mwaka huu.

Katika maazimio hayo, imekubaliwa Kambi ya Timu ya Taifa iwekwe mkoani Arusha kwa wachezaji wa mbio ndefu huku mbio fupi na za kati iwe Mkuza, Kibaha mkoani Pwani.

“Huu mwaka nataka uwe wa mafanikio makubwa kwa mchezo wa riadha na wanariadha watoboe kiuchumi mwaka huu…Hivyo kama viongozi tunataka kuandaa mazingira mapema ya kuwafanikishia hayo, ikiwemo kuwaweka kambini mapema kujiandaa na mashindano yenu, lakini pia tunataka mlete heshima ya utaifa katika mbio za kimataifa,” alisema Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Awali, wakitoa mapendekezo ya kambi iwe wapi, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Wanariadha Tanzania, Amani Ngoka, alisema kuwa kambi ya mbio ndefu kuanzia Kilomita 42 na 21 ziwe mkoani Arusha huku mbio fupi ziwekwe Pwani kwa ajili ya hali ya hewa kuruhusu mazoezi ya aina hiyo.

Mwanariadha Angelina Tsere wa JKT, alisema kuwa suala la kambi liwe wapi wataamua viongozi wenyewe na wao kama wanariadha watakwenda, kikubwa ni nidhamu, kujituma sambamba na kuheshimu ratiba ya kambi, ndivyo vinavyoweza kuleta mafanikio katika mazoezi na medali katika mashindano yoyote.

Naye Mwanariadha wa miruko mitatu, Michael Gwandu, alipendekeza kambi iwe Arusha kutokana na kuwa na hali ya hewa stahiki, sambamba na miundombinu rafiki kwa mazoezi na vifaa pia, huku akiiomba shirikisho hilo kuwa na mashindano ya mara kwa mara katika mchezo huo ambao unaelekea kusahaulika.

Kwa upande wake, Kocha mzoefu na Mjumbe wa Kamati ya Mbio za Barabarani na Nyika ya RT, John Bayo, alisema kuwa mafanikio ya kambi itakayowekwa Arusha ni mashindano ya mara kwa mara na wapinzani wao wakubwa katika mbio nchi jirani ya Kenya, ambao watakuwa wanaomba mashindano ya mara kwa mara kwa lengo la kuwajenga wanariadha kisaikolojia sambamba na kimashindano.

Akihitimisha mjadala huo, Mtaka alisema kwa mwaka huu RT imejipanga kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wanariadha, hivyo kambi hiyo ianze wiki ijayo mkoani Arusha kwa mbio ndefu na wanaokimbia mbio fupi wataweka kambi Pwani.

 “Kuna watu watakaoshangaa kwanini Arusha, lakini tunaangalia ni wapi kuna umaarufu wa Riadha ambayo inaweza kutupatia wadhamini kwa mwaka mwingine, maana kwa mwaka huu tayari fedha zipo.

Hivyo wachezaji sasa msiniangushe, bali pambaneni kuhakikisha mnaleta heshima ya nchi maana kisingizio hamtakuwa nacho,” alisema Mtaka.

Kwa upande wake Kocha mwandamizi, Thomas Tlanka wa Klabu ya Talent jijini Arusha, alisema kuwa wamefurahi kambi hiyo kuwekwa Arusha, kikubwa kwa sasa ni kupambana ili kuhakikisha wanariadha wanakuwa katika muda bora zaidi.

Aidha, alishauri RT kuchagua Kocha Mkuu mmoja huku wengine wakiwa wasaidizi.

Tukio kubwa litakaloanza ni Mbio za Nyika za Dunia ‘World Cross Country’ zitakazofanyika Machi 30 mwaka huu nchini Denmark, hivyo kitaifa maandalizi yataanza kwa mbio za majaribio kisha Mashindano ya Wazi ya Taifa Februari 16 mjini Moshi, ambako wachezaji watakachaguliwa timu ya Taifa wataingia kambini moja kwa moja kuendelea kujinoa na mashindano hayo ya Dunia.

No comments:

Post a Comment

Pages