WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea
leseni ya usajili wa chaneli ya utalii ya Tanzania Safari ambayo itaiwezesha kuoneshwa
kwa umma bila ya malipo yoyote (a must-carry channel) na wamiliki wa visimbusi.
Waziri Mkuu
amekabidhiwa leseni hiyo leo mchana (Jumatano, 16 Januari, 2019) kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa,
jijini Dodoma ambako alitaka apewe mrejesho kutoka kwa wajumbe wa Kamati Maalum
ya kusimamia uboreshaji wa Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel).
Akikabidhi
leseni hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba amesema
kukamilika kwa usajili huo kumeiwezesha chaneli hiyo ianze kuonekana kwenye
kisimbusi cha AZAM namba 109.
Akitoa
taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Rioba amesema Kamati hiyo iliundwa Desemba
21, mwaka jana na inajumuisha wajumbe kutoka taasisi ambata za maliasili na
utalii kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
“Baada ya
kupata leseni, sasa hivi tunaonekana kwenye kisimbusi cha AZAM chaneli namba
109 na pia kwenye intelsat ambako tutaweza kuonekana kwenye nchi zote barani
Afrika, sehemu kubwa ya bara la Ulaya na Uarabuni,” amesema.
Mapema, akichangia hoja kwenye kikao hicho,
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali (Mst.) Hamisi Semfuko
alisema chaneli hiyo inaweza kunufaika kwa kupata matangazo kutoka kwa wamiliki
wa mahoteli, makampuni ya kutoa huduma za utalii na wenye magari ya utalii.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Allan Kijazi alisema chaneli ya Tanzania Safari
imekuja katika wakati muafaka kwa kuwa itaongeza juhudi za taasisi zao
kutangaza vivutio vilivyopo nchini na hivyo kuongeza idadi ya watalii wa ndani
na wa nje.
“Uwepo wa chaneli hii utasaidia kuondoa
upotoshaji wa makusudi uliokuwa ukifanywa na baadhi ya nchi kuwa vivutio fulani
viko kwenye maeneo yao wakati siyo kweli,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
JUMATANO,
JANUARI 16, 2019.
No comments:
Post a Comment