*Asema Mkesha Mkubwa wa
Kitaifa mwaka huu utafanyika Dodoma
ASKOFU wa Kanisa
la Tanzania Fellowship of Churches (TFC), Dk. Godfrey Mallasy amesema Jiji la Dodoma
kwa sasa ni shwari na liko tayari kwa ujio wa Rais, Mheshimiwa Dk. John Pombe
Magufuli.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Februari 11, 2019) wakati
akizungumza na waandishi wa habari kwenye kanisa la Dodoma Christian Centre mara
baada ya kumaliza ibada maalumu ya kuombea ujio wa Rais Magufuli jijini Dodoma.
Askofu Mallasy alikuwa
akihitimisha semina ya siku nne ya jinsi ya kutambua madhabahu zinazokutesa na
kuzivunja na kisha kufunguliwa.
Alisema TFC iliandaa
semina hiyo kwa kushirikiana na makanisa mengine na kuamua kuhitimisha kwa
maombi ya kuvunja madhabahu za mkoa wa Dodoma na kujenga madhababu ya kitaifa.
“Ndoto ya Serikali
kuhamia Dodoma inakaribia kutimia kwa sababu wizara zote zimeshahamia hapa na
Mheshimiwa Rais wetu anakaribia kuhamia. Kwa hiyo, viongozi wa kiroho tunao
wajibu wa kumuandalia makazi yake ya kiroho. Jambo lolote likitokea, basi ujue
limeanzia rohoni,” alisema.
“Leo tuko Dodoma,
madhabahu ya hapa inasema kila kitu kitadidimia (kutokana na asili ya neno
Dodoma – idodomya- linalomaanisha kudidimia). Na falme za hapa zimetamka hilo
lakini baada ya maombi haya, sisi tunasema Dodoma haitadidimia, bali itaamka.”
Alisema maneno hayo kupinga
hali ya uduni wa Dodoma, yanaendana na ujasiri wa Serikali ya awamu ya tano
kuhamishia shughuli zake zifanyike makao makuu ya nchi, Dodoma.
“Rais wetu anakuja hapa
na ana ndoto kubwa, je ndoto hizo zitaenda wapi? Jeshi la Mungu liko hapa, kwa
hiyo ndoto hizo hazitadidimia kama jina lilivyo. Kupitia kuangusha ngome na madhababu
za Dodoma, mambo yanaenda kubadilika,” alisisitiza.
Alisema maombi hayo
yamefanyika ili Rais Magufuli aweze kutawala kwa amani na kutekeleza ndoto zake
za kuijenga Tanzania mpya kwa mafanikio makubwa. Alisisitiza Watanzania wote, kuanzia
kwenye ngazi ya familia, waendelee kuliombea Taifa liwe na amani kwa sababu
pasipokuwa na amani, hakuna kinachoweza kufanyika.
Mapema, katika
ibada hiyo, Askofu Mallasy aliwaongoza wachungaji wengine 20 wa TFC kutoka
mikoa mbalimbali nchini pamoja na wachungaji kutoka makanisa ya FPCT, EAGT,
TAG, KKKT na Anglikana kuimba wimbo wa Taifa na kufanya kitendo cha kumpokea
Rais Magufuli.
Pia aliongoza waumini mbalimbali waliohudhuria ibada hiyo kuvunja
madhabahu kwenye mihimili yote mitatu ya nchi yaani mahakama, Bunge na Serikali
kwa kutaja wizara mbalimbali, kuwaombea wakuu wa mikoa yote, wilaya zote, wakurugenzi
wa halmashauri zote za Majiji, miji, manispaa na wilaya.
Wakati huohuo,
Askofu Mallasy ametangaza kwamba Mkesha
Mkubwa wa Kitaifa ambao hufanyika tarehe 31 Desemba kila mwaka kwa ajili ya
kuliombea Taifa, mwaka huu utafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Mkesha wa kuliombea
Taifa, umekuwa ukifanyika nchini kila mwaka kuanzia mwaka 1997.
No comments:
Post a Comment