HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 17, 2019

KILIMO WEZESHENI WATAFITI WA MICHIKICHI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama mbegu ya mchikichi inayoonyesha tabaka la  mafuta wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Kilimo Mwandamizi na Mratibu wa Utafiti wa Kilimo mkoani Tabora na Kigoma, Dkt. Filson Kagimbo (kulia) wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha  Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. Wapili kushoto ni mkewe Mary. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mikungu ya mchikichi iliyochavushwa kitlaam ili kupata mbegu bora wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti wa Michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, Februari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


KIGOMA, TANZANIA
 
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iwawezeshe watafiti katika kituo cha Utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma ili waweze kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo.

Amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu kwenye zao hilo la michikichi, hivyo Wizara ya Kilimo haina budi kukiwezesha kituo hicho kwa lengo la kuzalisha mbegu bora zitakazosambazwa kwa wakulima.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 17) wakati alipotembelea kituo cha Kihinga kwa ajili ya kukagua shughuliza uzalishaji wa mbegu za michikichi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Amesema Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya sh. bilioni 600 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

“Wizara ya Kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama yalivyofanya Mataifa mengine ya Costa Rica na Malaysia.”

Amesema wakulima wa zao hilo wanahitaji kupata mafanikio, hivyo kituo hakina budi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora. Ili wafikie malengo amewasahauri washirikiane na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu.

Pia Waziri Mkuu amesema chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga, kiendelee kutoa elimu na Wizara ya Kilimo ijenge majengo yake inayoyahitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli za utafiti. Eneo la chuo linaukubwa kwa hekta 920.

Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kwa mikoa ya Tabora na Kigoma, Dkt. Filson Kagimbo amesema michikichi iliyopo sasa inauwezo wa kuzalisha tani 1.6 ya mawese kwa hekta moja ambao kidogo na hauna tija.

Amesema mbegu wanazozizalisha zinalenga kumuongeza tija mkulima kwa kuwa zitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani nne kwa hekta, pia wanaendelea kuangalia vinasaba vya mbegu vilivyopo ili wazalishe mbegu bora zaidi.

“Tutakusanya vinasaba vyote vya mbegu tulivyonavyo na kuvitathimini na kuona uwezo wake na ikibidi tutaagiza kutoka nje ya nchi ili kuboresha zaidi.” Miche ya michikichi inachukua muda wa miezi 18 kutoka hatua ya uchavushaji hadi kusambazwa kwa wakulima.

Baada ya kumaliza shughuli ya ukaguaji wa uzalishaji wa mbegu kituoni hapo, Waziri Mkuu alikagua shamba la michikichi la Gereza la Kwitanga  lenye ukubwa wa ekari 400 na kupanda mche kama ishara ya uzinduzi wa upandaji wa miche bora shambani hapo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu katika zao hilo na inategemea taasisi zake mbili za Jeshi la Magereza (Kwitanga) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT-Bulombora), ambazo zinamashamba makubwa ya michikichi.

Kadhalika Waziri Mkuu ameagiza elimu kuhusu kilimo cha zao la michikichi kuanzia hatua za awali hadi uzalishaji wa mafuta itolewe mashuleni ili wanafunzi waanze kupata ulewa na ifikishwe hadi kwa wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 17, 2019.

No comments:

Post a Comment

Pages