NA Mwandishi Wetu
KWA kutambua umuhimu na ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania,
serikali imeiahidi kampuni ya mawasiliano ya Halotel kuendelea
kushirikiana nayo katika kutatua changamoto wanazozikabili kwa pamoja.
Hayo
yalisemwa wakati wa ziara maalum ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na
Uchukuzi, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati alipoitembelea kampuni hiyo
ili kujua shughuli wanazozifanya katika kuwahudumia wateja pamoja na
changamoto wanazokumbana nazo kila siku.
“Lengo
la ziara hii ni kuja kuwasikiliza, kujua shughuli mnazozifanya pamoja
na changamoto mnazokumbana nazo. Serikali inatambua ukuaji na umuhimu wa
sekta ya mawasiliano katika kuchangia uchumi.
Na wadau wakubwa katika
sekta hii ni makampuni ya simu kama Halotel. Hivyo hatuna budi
kuyatembelea, kuongea nayo, kuyasikiliza na kushirikiana nao wapi
tufanye kipi kama serikali katika sekta nzima ya mawasiliano. Ningependa
kuwatoa hofu kwamba kama serikali tuko pamoja nao,” alisema Mhandisi
Nditiye.
“Serikali
inatambua sana mchango wa makampuni ya simu na ndiyo maana tumeamua
kuwatembelea ili kujua shughuli wanazozifanya. Kwa mfano, mbali na
kuzungumza na kusikiliza changamoto zao lakini nimepata fursa ya
kutembelea kitengo chao wanacho hudumia wateja, mitambo na kitengo chao
wanakitumia kufanyia huduma za kifedha. Nimezisikiliza changamoto zao na
ninaahidi kwenda kuzifanyia kazi,” alihitimisha Mhandisi Nditiye.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halotel Nguyen Van Son, aliezea mafanikio
ambayo kampuni yake imeyafikia mojawapo ikiwa ni ahadi ilizozitoa kwa
serikali katika utoaji wa huduma nchini.
“Katika
utoaji wa huduma za mawasiliano Tanzania tulitoa ahadi kadhaa kwa
serikali na ningependa kuchukua fursa hii kuifahamisha serikali kuwa
tumetekeleza kwa kiasi kikubwa. Tuliahidi kutoa huduma za mtandao wa
intaneti katika shule 450 na tumevuka lengo kwa 455. Tuliahidi kutandaza
kebo za huduma ya intaneti katika ofisi za mabaraza ya wilaya 150 na
tumefanikiwa kwa kufikia ofisi 147.
Pia kusambaza miundombinu ya
mawasiliano ya fibre katika hospitali za wilaya 150 na tumefanikiwa zote
150. Tuliahidi kusambaza miundombuni ya mawasiliano ya fibre kwa vituo
vya polisi vya wilaya 150 na tumefanikiwa 121. Lakini pia, tuliahidi
kusambaza miundombinu ya mawasiliano ya fibre katika vituo vya ofisi za
posta za wilaya 65 na tumevuka kwa kufunga 66,” alisema na kuongezea
Son.
Licha
ya mafanikio hayo ambayo Halotel imeyafanikisha kwa kutimiza ahadi
ambazo iliipatia serikali, kampuni hiyo ilielezea changamoto kadhaa
inazokumbana nazo.
“Ili
kutimiza dhima yetu ya kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma
za mawasiliano kwa bei nafuu lakini pia tunakumbwa na changamoto kadhaa.
Mojawapo ni pamoja na kuharibiwa kwa mifumo yetu ya miundombinu ya
mawasiliano na baadhi ya wananchi ambao sio waaminifu katika baadhi ya
mikoa.
Vitendo hivi si tu vinakwamisha juhudi zetu za kufikisha
mawasiliano katika kila pembe ya nchi lakini pia inawazuia wananchi
kufikiwa na huduma zetu hivyo kukwamisha shughuli za mawasiliano na
uchumi. Tungeomba katika hili serikali kushirikiana nasi ili kuzuia
vitendo hivi vya kihalifu na kujenga hamasa juu ya umuhimu wa mitambo
hii,” aliongezea Son.
“Pia
tunaiomba serikali kushirikiana na Halotel katika kupambana na
changamoto ya wizi wa mitandaoni. Kama mnavyojua huduma za mawasiliano
hususani huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi yanatumika kwa
kiasi kikubwa katika kurahisisha shughuli mbalimbali. Wahalifu wa
mitandaoni nao wanaoitumia fursa hii kuwalaghai wateja hivyo kuvunja
uaminifu baina yetu.
Halotel inapendekeza kuwepo na ushirikiano na
serikali katika kulikabili hili na kulitatua kwa pamoja. Tunapendekeza
kuwepo kwa vikao, semina au warsha za mara kwa mara ili kupanga mikakati
na kumaliza kabisa changamoto hii,” alihitimisha Son.
Makamu
wa Kitengo cha Idara ya Umeme wa Kampuni ya Halotel, akitoa maelezo
jinsi mfumo wa Umeme unavyofanya kazi kwenye kituo cha data kwa Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye
(kushoto) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Nguyen Van Son wakati wa
ziara ya kikazi ya Naibu waziri huyo katika ofisi za makao makuu za
Halotel jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu dhima ya ziara aliyoifanya kwa
ofisi za Makao Makuu ya Halotel jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Nguyen Van Son.
No comments:
Post a Comment