Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E Mwangela akisaini kitabu cha wageni ofisi
ya TANESCO Songwe wakati alipoenda kufahamu mpango wa kumaliza matatizo ya
umeme mkoani hapa, Kushoto kwake ni Kaimu Meneja TANESCO Mkoa wa Songwe,
Aristidia Clemence.
SONGWE, TANZANIA
Shirika la Umeme Nchini
TANESCO Mkoa wa Songwe limepewa siku tatu kuandaa mkakati utakaoeleza namna ya
kumaliza matatizo ya umeme ikiwemo katizo la mara kwa mara la umeme na tatizo
la kiwango kidogo cha umeme.
Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E Mwangela ametoa agizo hilo mapema leo asubuhi alipofika
ofisi za TANESCO Songwe kufuatia kukatika mara kwa mara kwa umeme na pia kila
siku ya Jumamosi ambapo alimtaka Meneja wa shirika hilo kueleza mkakati wa
kumaliza tatizo hilo.
“Nimekuja hapa
kwakuwa naona sasa tunageuka makubaliano ya kukata umeme kila jumamosi tu, sasa
katikati ya wiki umeme unakatika sana, lakini hata hayo makubaliano ya jumamosi
naona muda unaenda tu hatujui lini mtakamilisha matengenezo mnayoyafanya kila
Jumamosi”, Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Ameongeza kuwa Mkoa
unapata athari kubwa kufuatiwa kutokuwepo umeme wa uhakika kwakuwa shughuli za
uzalishaji viwandani, shughuli za majumbani zinazohitaji umeme na hata baadhi
ya huduma za kijamii zinazohitaji uwepo wa umeme wa uhakika zinaathiriwa huku
akielezea kuwa wananchi hawapewi taarifa.
“Nawaelekeza kuanzia
sasa mkizima umeme au hata ikitokea hitilafu taarifa na sababu zitolewe ili
ifahamike umeme umekatika kwa sababu zipi, tatizo la umeme kwetu limeshakuwa
kero kubwa kwani hakuna maendeleo
hususani ya viwanda bila umeme”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela. amewataka TANESCO Songwe waongeze
ujuzi na maarifa kutoka kwa maeneo mengine ambao wameweza kutatua matatizo kama
hayo pia wafahamu mahitaji ya vifaa vinavyotakiwa kwa ajili ya matengenezo wanayoyafanya.
Naye Kaimu Meneja
TANESCO Mkoa wa Songwe Aristidia Clemence amesema kuwa kukatika umeme mara kwa
mara kunatokana na Mvua zonazoendelea kunyesha kwani husababisha nguzo kuanguka
na pia radi hupasua vikombe katika nguzo.
Amesema matatizo ya
Umeme Mkoa wa Songwe yataisha pale ambapo Mradi wa Umeme wa Gridi ya Taifa kutoka
Iringa mpaka Nkangamo Momba, wa Kilovoti 400 utakapokamilika kwani kwa sasa
umeme unaopatikana ni mdogo na unapatikana kwenye laini moja yenye Zaidi ya
Kilometa 1200 tofauti na mikoa mingine yenye line kumi na umeme wa kutosha.
“Hata sisi tunaumia
umeme unapokatika kwani tunatambua umuhimu wa umeme na ndio maana tunafanya kazi
usiku na Mchana, Mkoa huu ulikuwa na matatizo ya nguzo chakavu pia baadhi ya
vikombe vimeharibika ndio maana kila jumamosi tunazima umeme ili kubadilisha
nguzo na vikombe hivyo”, ameeleza Clemence.
Clemence ameongeza
kuwa kwa sasa kuna ujenzi wa switching
station ambao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kusaidia endapo kuna
hitilafu imetokea sehemu moja umeme usikatike mkoa mzima tofauti na sasa ambapo
hitilafu ikitoa wilaya moja mkoa mzima unakosa umeme.
“Pia tatizo lililopo
sasa ni hitilafu ikitokea mkwajuni Songwe umeme ukikatika ni Mkoa Mzima ila
ujenzi huu wa Switching Station
utasaidia kuondoa tatizo hilo, pia mradi ule wa Iringa wa Gridi ukikamilika
matatizo ya umeme yatakwisha hivyo nawasihi wenye viwanda na wenye nia ya
kuwekeza kwenye viwanda wasikate tamaa”, amefafanua Clemence.
Kwa upande wao
wananchi Mkoani Songwe wameiomba serikali iwasaidie uwepo wa umeme wa uhakika
ili waweze kuzalisha na kufanikisha uchumi wa viwanda, aidha wamesema kukatika
kwa umeme mara kwa mara kunaathiri upatikanaji
wa huduma za kijamii kama vile baadhi ya huduma za afya hospitalini
No comments:
Post a Comment