HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2019

Washindi wa fainali NMB MastaBata watangazwa


 Mtangazaji wa EFM, Emmanuel Kapanga, akizungumza na mmoja wa wateja wa Benki ya NMB aliyejishindia Safari ya kwenda Dubai. Kushoto ni Saum Adadi kutoka Selcom na kulia ni Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abdallah Hemed.
Mtangazaji wa EFM, Emmanuel Kapanga, akizungumza na mmoja wa wateja wa Benki ya NMB aliyejishindia Safari ya kwenda Dubai. Kushoto ni Tunu Hassan wa EFM Radio na kulia ni Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Abdallah Hemed.
 Meneja Mwandamizi wa Biashara za Kadi, Manfredy Kayala, akizungumza katika droo ya mwisho ya Masta Bata. Kulia ni Philbert Casmir. Katikati ni Stephen Jilala.
 Meneja Mwandamizi wa Biashara za Kadi, Stephen Jilala akizungumza na waandishi wa habari wakati wa droo ya mwisho ya Masta Bata. Kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Biashara za Kadi, Manfredy Kayala. Kulia ni Philbert Casmir. 


NA MWANDISHI WETU

SHINDANO la matumizi ya kadi za Masterpass na Mastercard lililoratibiwa na Benki ya NMB, lijulikanalo kama NMB MastaBata, limefikia tamati leo Ijumaa Februari 22 kwa washindi watatu wa tiketi za safari iliyolipiwa kila kitu kwenda Dubai kutangazwa.

Droo ya kuwapata washindi hao ilifanyika Makao Makuu ya Benki ya NMB, chini ya usimamizi wa mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (TGB), Abdallah Hemed, ambako washindi waliopatikana wanaanza maandalizi binafsi kwa ajili ya safari hiyo.

NMB MastaBata ni promosheni iliyodumu kwa miezi miwili tangu ilipozinduliwa Desemba mwaka jana, ikilenga kuchagiza matumizi ya kadi za Masterpass QR na Mastercard miongoni mwa wateja wa NMB, huku zawadi kadhaa zikiwamo za pesa na simu ‘smartphone.’

Washindi watatu walioshinda katika droo ya leo ni Eistein Ngao wa Kawe Dar es Salaam ambaye ni Mfamasia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Magebo Simon wa Arusha ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa huo na Paul Kasambala, mkazi wa Pugu Kajiungeni Dar es Salaam.

Baada ya kupigiwa kwa nyakati tofauti na kutangazwa washindi, Ngao, Magebo na Kasambala ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania walikiri kufurahishwa na ushindi huo na wakawachagua wake zao kuambatana nao wakati wa safari hiyo.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa washindi hao, Meneja wa Kadi wa NMB, Stephen Jilala, alisema wanajiskia faraja kukamilisha shindano hilo la miezi miwili, lililowazawadia pia pesa taslimu washindi 140 (Sh. 100,000 kila mmoja).

Ukiondoa washindi wa safari ya Dubai (Aprili mwaka huu) na waliojishindia fedha taslimu, NMB MastaBata pia lilitoa washindi 12 waliojibebea simu janja ‘smartphone’ aina ya Samsung Galaxy S9+ katika kipindi chote cha kinyang’anyiro hicho. 

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kadi wa NMB, Philbert Casmir, alisema mwitikio wa matumizi ya kadi za Masterpass na Mastercard miongoni mwa wateja wa NMB ulikuwa mkubwa na kwamba wateja wao wataendelea kupata huduma bora kutoka benki hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages