WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameitaka Benki ya Biashara nchini (NBC) iongeze wigo wake ili iweze
kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Ametoa wito huo leo
(Alhamisi, Februari 14, 2019) wakati
akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi ofisini
kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Ninatoa wito kwenu
mpanue wigo katika utoaji wa huduma zake hapa nchini ili kuwawezesha wananchi
wengi zaidi kuhifadhi fedha zao katika eneo salama,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema wakati
Serikali ikiendelea kuhamasisha wananchi waongeze nguvu katika sekta ya kilimo,
taasisi za fedha hazina budi kusogeza huduma zao karibu na wananchi ili waweze
kutunza fedha zao katika hali ya usalama badala ya kuzihifadhi majumbani.
Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kuipongeza benki ya NBC kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za
kuwawezesha wananchi kupitia mikopo kwa wajisiriamali wadogo ambayo
inawawezesha kuongeza mitaji yao ya biashara mbalimbali.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi huyo wa NBC amesema ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea
mazingira
mazuri ya kufanya biashara na mwaka wa fedha uliopita wamefanikiwa
kutengeneza
faida na kwamba wanatarajia kutoa tena gawio. Hata hivyo, hakutaja ni
kiasi gani cha gawio kitatolewa, kwa sababu anasubiri uamuzi wa Bodi.
Pia amemkabidhi
Waziri Mkuu hundi yenye thamani ya shilingi 11,270,000 ambazo amesema
zitasaidia katika ujenzi wa kituo cha polisi wilayani Ruangwa.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, FEBRUARI 14, 2019.
No comments:
Post a Comment