MAANDALIZI ya Timu ya
Taifa ya Mbio za Nyika kuelekea mashindano ya Dunia yatakayofanyika mjini Arhus
Denmark Machi 30 mwaka huu yanaendelea vema.
Timu hiyo ya Taifa
iko kambini jijini Arusha chini ya ufadhili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), ikijiwinda vilivyo kuelekea mashindano hayo.
Kwa mujibu wa Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, maandalizi
kuelekea mashindano hayo yamekamilika kwa asilimia takribani 95.
Gidabuday, alisema
wakati timu ikiwa kambini jukumu kubwa lilikuwa ni kushughulikia taratibu za
ushiriki ikiwamo masuala ya pasi za kusafiria na viza za kuruhusu kuingia nchini
Denmark.
“Tunashukuru zoezi
hili ambalo lilikuwa gumu tumelikamilisha na leo kundi la mwisho la wachezaji
wetu limekamilisha masuala ya viza na limerejea Arusha kuendelea na mazoezi,”
alisema Gidabuday na kuongeza.
Masuala ya pasi za
kusafiria imekuwa changamoto sana kwa vijana wetu, maana vijana wengi upande wa
Junior walikuwa hawana pasi na viambatanisho ambavyo vingewawezesha kupata pasi
hizo kwa haraka, jambo ambalo liliwafanya baadhi kuchelewa masuala ya usajili,
lakini limetupa fundisho.
Gidabuday, alisema
kutokana na hali hiyo shirikisho limeamua kuchukua hatua za kuendelea
kuwatafutia pasi za kusafiria kwa faida ya baadaye, ili pale watakapopata fursa
ya kuiwakilisha nchi kimataifa pasiwepo na tatizo hilo tena.
Katibu huyo, alisema
baada ya kukamilisha masuala ya viza, timu inaendelea na mazoezi ya mwisho
mwisho kabla ya kuagwa rasmi Machi 27 jijini Arusha na siku hiyo hiyo usiku
kukwea pipa kwenda Denmark kupeperusha bendera ya Taifa.
Alisema, mgeni rasmi
katika hafla hiyo kuagwa timu watamtangaza hivi karibuni taratibu
zitakapokamilika.
Aliongeza kuwa, wana imani na maandalizi yaliyofanyika yatazaa matunda
katika mashindano hayo na kuipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro
na DStv kwa sapoti kubwa waliyoitoa kufanikisha maandalizi hayo.
Gidabuday, alisema
msafara wa Tanzania katika mashindano hayo utakuwa na wachezaji 16 na viongozi
ukiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais- Ufundi RT, Dk. Hamad Ndee.
Viongozi wengine ni Kocha
Mkuu Meta Petro, Kocha Msaidizi Madai Jambau na Matron Marcelina Gwandu.
Wachezaji kwa upande
wa wanaume ni Marko Monko, Joseph Panga ‘Mti Mkavu’, Faraja Damas, Emanuel
Giniki, Gabriel Geay, Francis Damiano na Yohana Elisante.
Wanawake ni Failuna Matanga,
Magdalena Shauri, Angelina Tsere, Sisilia Ginoka, Mayselina Mbua, Amina Mgoo, Anastazia
Dolomongo, Aisha Magelani na Natalia Elisante.
No comments:
Post a Comment