HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 21, 2019

WAZIRI LUVKUVI AMSIMAMISHA AFISA ARDHI KANDA YA KASKAZINI

NA MBARUKU YUSUPH, TANGA
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Willium Lukuvi amemsimamisha kazi afisa ardhi wa kanda ya kaskazini Thadeus Dominic Riziki  baada ya kuuza shamba la Amboni Estate lililopo jijini Tanga kinyume na utaratibu.
Hatua hiyo imechukuliwa na Waziri huyo jana wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wananchi na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa jiji la Tanga uliofanyika katika viwanja vya Tangamano Mkoani Tanga.
Lukuvi alisema kuwa Afisa ardhi kanda hiyo wakati akiwa na cheo cha afisa ardhi wa Jiji la Tanga aliuza shamba la Amboni kwa mwekezaji huku sheria ikielielekeza shamba hilo liwekwe katika utaratibu wa kufutiwa hati na Rais .
“Namsimamisha kazi Ofisa huyo ambaye hivi juzi amepandishwa na kuwa afisa kanda kutokana na kubariki mauziano ya shamba ambalo lilitakiwa kufutwa”alibainisha Waziri Lukuvi.
Katika hatua nyingine Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuiagiza Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha shamba hilo linarudi mikononi mwa serikali kwa ajili ya kuanza taratibu za kulifutia hati.
Alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa jiji hilo kuhakikisha wanasimamia sheria na taratibu za ardhi kama zinavyoelekeza badala ya kuendelea kufanya kazi kwa malalamiko bila ya kuchukuwa hatua stahiki.
Alisema Tanga Jiji inamaeneo mengi ya mashamba ambayo yameshindwa kuendelezwa huku kukiwa na utendaji mbovu wa kuyafuta mashamba hayo ili Rais Magufuli aweze kuridhia na kuyagawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Aidha katika kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ilionyeshwa kuwa kesi nyingi zinatokana na wananchi wengi kuchukuwa fidia ili hali wakiwa hawajui thamani ya maeneo yao.
Sambamba na hayo Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa aliwataka wakazi wa Jiji la Tanga kuwasilisha kero zao za ardhi kwa waziri huyo kwani yupo kwa ajili ya kuhakikisha anatatua migogoro iliyopo.
Alisema Serikali ya Rais Magufuli ni ya hapa kazi tuu hivyo aliwaomba wananchi kueleza kero zao ambazo ni za ukweli ili Waziri aweze kuzifanyia kazi kwa haraka.

No comments:

Post a Comment

Pages