NA
MWANDISHI WETU
KIKOSI cha Timu ya Tanzania inayotarajiwa
kushiriki michezo ya Vijana ya Kamati za Olimpiki Afrika (ANOCA), Zone 5 jijini
Kigali Rwanda, imeondoka jijini Dar es Salaam jana ikiwa na matumaini kibao.
Timu hiyo inayoundwa na michezo ya Kikapu na
Riadha, iliondoka jana amjira ya saa 11:30 jioni na ndege ya Shirika la Rwanda,
ikiwa chini ya Mkuu wa msafara, Shehe Mohamed Ali kutoka KMKM Zanzibar.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kukwea pipa,
Kocha wa Riadha, Mwinga Mwanjala, alisema vijana wake wanakwenda kupambana
kadiri ya walivyojiandaa.
“Tunakwenda kupambana kulingana na jinsi
tulivyojiandaa, tusubiri siku ya tukio tuone vijana wanaamkaje, tuombe vijana
wawe na afya njema wapambana kadiri ya uwezo wao ili kufanya vizuri,” alisema
Mwinga.
Naye Kocha msimamizi wa timu ya Kikapu, Phineas
Kahabi, alisema walikuwa kambini kituo cha michezo cha Filbert Bayi, Mkuza
Kibaha hadi jana na wamejiandaa vema.
“Tulikuwa na muda mwingi wa kujiandaa, vifaa na
huduma ikiwamo malazi ilikuwa nzuri…Shukrani kituo cha Filbert Bayi na Kamati
ya Olimpiki kwa ujumla, vijana wako vizuri mentally na physically, hivyo hatuna
visingizio,” alisema Kahabi.
Kocha huyo, alifafanua kuwa kikosi chake
kinaundwa na wachezaji wanne na wanakwenda kucheza mchezo wa wachezaji watatu watatu ‘3x3’ huku wakitumia nusu kiwanja.
Kahabi, alitoa hofu Watanzania kuhusiana na
mchezo huo ambao bado haujaenea sana hapa nchini, kwamba vijana wake
walishaanza kuucheza toka mwaka jana, hivyo wamejiandaa kimwili na kiakili na
kwamba amekuwa akiwakumbusha mara kwa mara sheria za mchezo huo, kwani ni tofauti
na zile za Kikapu za kawaida.
Timu hiyo inaundwa na Wanariadha Regina
Mpigachai (Mita 800), Amos Matondo (Mita 400), Esther Martin (Mita 1,500), na
Gaudensia Maneno (Mita 800).
Kwa upande wa Kikapu ni Daud Maiga (Nahodha),
Josephat Sanka, Ally Abdallah na Charles Mayombo.
No comments:
Post a Comment