Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA
na wapenzi wa michezo kwa ujumla wametakiwa kujitokeza kwa wingi
kujisajili mbio za Ngorongoro ‘Ngorongoro Race 2019 - Half Marathon’
zinazotarajiwa kurindima Karatu mkoani Arusha, Aprili 20 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Muandaaji, Meta Petro kutoka Meta Sports Promotions,
maandalizi yanakwenda vema na mbio za mwaka huu zitakuwa na msisimko wa
hali yake.
Alisema
taratibu za usajili tayari zimeanza na walio mbali na Karatu na Arusha
wanaweza kujisajili kwa njia ya mtandao wa simu, M-Pesa 0754 82 13 80
(Meta Petro Bare).
Meta,
alisema pia usajili unafanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha,
Ofisi za Gidabuday Sports Foundation jengo la Namvua Plaza jijini Arusha
na Ofisi za Ngorongoro Race mjini Karatu.
Ngorongoro Race 2019 inashirikisha mbio za Kilomita 21 ‘Half Marathon’, Kilomita 5 ‘Fun Run’ na Kilomita 2.5 maalumu kwa watoto.
“Maandalizi
yanakwenda vema na tunatarajia washiriki zaidi ya 2,000 mwaka huu,
hivyo tunatoa rai kwa wakimbiaji kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje
ya nchi kuwahi kujisajili mapema kwani zoezi litafungwa rasmi Aprili 15
mwaka huu,” alisema Meta.
Alisema
kuwa mbio za mwaka huu, zitashirikisha wanariadha wengi kutoka ndani na
nje ya nchi kutokana na uamasishaji uliofanywa na waandaaji, ambao pia
wameahidi kuongeza zawadi kwa washindi.
Alibainisha
kuwa, mbali na zawadi kwa washindi, wakimbiaji 1,000 wa kwanza
watakaofanikiwa kumaliza mbio, kila mmoja atapewa medali yake ya
ushiriki.
Muandaaji
huyo, alisema medali hizo zinatarajiwa kutua nchini wakati wowote
kuanzia sasa kwa ajili ya mbio hizo, ambazo zitaanzia Lango Kuu ya
kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia kwenye
viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.
“Namba
kwa wanaotaka kushiriki mbio za kilomita 21 zitatolewa kwa Sh. 20,000
wakati zile za kujifurahisha za kilomita 5, zenyewe zitatolewa kwa Sh.
10,000 na watoto watapewa namba baada ya kutoa Sh. 5,000,” alisema na na
kuongeza.
Wameamua
mwaka huu kutoa namba kwa watoto kwa gharama ya Sh. 5,000, ili
kuwafanya watoto hao kuwa makini na mbio hizo na sio kushirikisha lundo
la watoto, ambao hawajajiandaa kwa lolote.
Alibainisha
kuwa, tayari shule zaidi ya tano za jijini Arusha zimethibitisha
kupeleka zaidi ya watoto 100 katika mbio hizo za mwaka huu, ambazo
watoto watakimbia kilometa 2.5.
Akizungumzia
maandalizi kwa ujumla, Petro alisema kuwa yanaenda vizuri na
wanatarajia kila kitu kitakuwa tayari siku chache kabla ya Aprili 20,
ambayo ni siku yenyewe ya mbio hiyo.
Mbali
na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika michezo na kuimarisha
ushirikiano, Ngorongoro Race inahamasisha utamaduni wa kutembelea
vivutio vya nchi na kupiga vita ujangili.
No comments:
Post a Comment