Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)
(katikati) akifurahia jambo lililozungumzwa na Makamu wa Rais wa Benki
ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem (hayuko
pichani) wakati wa mkutano wa ujumbe wa Tanzania na uongozi wa Benki
hiyo Mjini Washington D.C, Marekani. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar Bw. Khamis Mussa Omar
na kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kushoto) akiteta jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Bella Bird mara baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, Mjini Washington D.C nchini Marekani.
Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kushoto) akiteta jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Bella Bird mara baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, Mjini Washington D.C nchini Marekani.
Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C
BENKI ya Dunia imeahidi
kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu na msaada wenye thamani ya dola za
Marekani bilioni 1.7 sawa na takriban shilingi trilioni 4 kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi
cha mwaka wa fedha 2019/2020.
Ahadi hiyo imetolewa mjini
Washington D.C nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia
Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe
wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.
Bw. Ghanem amemhakikishia
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba uhusiano kati ya Serikali na
Benki yake bado uko imara na kwamba benki hiyo iko tayari kushirikiana na
Tanzania ili iweze kufikia maendeleo yanayo tarajiwa.
Miongoni mwa miradi
itakayonufaika na mkopo na msaada huo ni mpango wa elimu ambapo benki hiyo
imeongeza ufadhili kutoka dola milioni 300 hadi dola milioni 400 na mradi wa
kusaidia kaya masikini kupitia TASAF ambapo benki hiyo imeamua kuongeza kiwango
cha fedha kutoka dola milioni 300 hadi kufikia dola milioni 450.
Kiasi kingine cha fedha
kitatumika kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara,
maji, Tehama, Afya, kilimo, hifadhi ya jamiim Nishati, utawala bora, lishe,
sekta ya fedha, biashara, mazingira na maliasili pamoja na maji nk.
Akizungumza kwenye kikao
hicho Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Benki hiyo
namna inavyoisaidia nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambapo
mpaka sasa Benki hiyo imefadhili miradi 21 ya maendeleo kwa gharama ya dola za
Marekani bilioni 4.8, sawa na takriban shilingi trilioni 11.
Ameahidi kuwa Serikali ya
Tanzania itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika
utekelezaji wa masuala mbalimbali na kuiomba benki hiyo iendelee kuisaidia nchi
ili iweze kufikia maendeleo yaliyokusudiwa ikiwemo kuondoa umasikini wa wananchi.
Ujumbe wa Tanzania
ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, ukimshirikisha pia Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, upo mjini Washington D.C nchini Marekani
kuhudhuria mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF,
taasisi ambazo Serikali ina hisa.
No comments:
Post a Comment