Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
alipokuwa akijibu swali la msingi bungeni mjini Dodoma.
Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa kwa sasa nchi
haina tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko kutokana na hatua
mbalimbali ilizozichukua kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuongeza ukwasi
kwenye uchumi.
Hayo yameelezwa leo Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Momba Mhe. David Silinde (Chadema),
aliyetaka kujua sababu za mzunguko mdogo wa fedha.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, katika
kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko, Serikali
kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ikiwemo
kushusha riba ya Benki Kuu (discount rate)
kutoka asilimia 16 kwa mwezi Machi, 2017 hadi asilimia 7, Agosti 2018.
“Benki Kuu ilipunguza kiwango cha
kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na mabenki ya
biashara(Statutory Minimum Reserve
Requirement, (SMR)) kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 mwezi April 2017
pamoja na kuruhusu mabenki kutumia asilimia 10.0 ya sehemu ya SMR kama chanzo
kimojawapo cha kusaidia hali ya ukwasi kwenye uchumi”, alisema Dkt. Kijaji.
Alisema Benki Kuu ilianzisha
utaratibu wa kutoa mikopo ya muda maalumu kwa mabenki pamoja na kununua fedha
za kigeni kutoka kwenye soko la jumla la mabenki ili kuongeza ukwasi kwenye
uchumi.
Alifafanua kuwa mzunguko wa fedha
katika uchumi unaendana na malengo pamoja na mahitaji halisi ya shughuli za
kiuchumi zizopo kwa sasa.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema Serikali
kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza Sera ya Fedha inayolenga kusimamia
mzunguko wa fedha unaoendana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la
kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji
wa uchumi.
No comments:
Post a Comment