Na Idara ya Habari-NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani
kwenye kata sita (6) zilizopo kwenye halmashauri sita (6) katika mikoa sita (6)
ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesema Jijini Dar
es Salaam leo (Jumanne 09.04.2019) kwamba uchaguzi huo utafanyika tarehe 19 Mei
mwaka huu.
Akisoma taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume, Jaji Kaijage amesema
kwamba fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya tarehe
15 hadi tarehe 19, Aprili mwaka
huu.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Tume
amesema kwamba uteuzi wa wagombea pia utafanyika tarehe 19, Aprili mwaka huu na kampeni za uchaguzi
zitafanyika kuanzia tarehe 20, Aprili hadi tarehe 18 Mei mwaka huu.
Alifafanua kwamba uchaguzi katika kata hizo, utafanyika sambamba na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la
Arumeru Mashariki.
“Tume inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi
kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo
yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi
huu mdogo,” alisema Jaji Kaijage.
Awali Jaji Kaijage alisema kwamba maamuzi ya kutangaza uchaguzi kwenye
kata hizo yamefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri
mwenye dhamana na Serikali za Mitaa
ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya
Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wazi
wa nafasi hizo.
Alisema kwamba nafasi hizo wazi zimetokana na vifo vya Madiwani watano
(5) na mmoja (1) kujiuzulu.
Kata hizo ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani
Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Mikocheni
iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Mvuleni
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi na Manda iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment