HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 13, 2019

Simba kuitafuna TP Mazembe leo


Kikosi cha Simba



NA JOHN MARWA
HAKUNA namna lazima kieleweke! Unaweza kusema kuelekea katika mchezo wa leo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), kati ya wenyeji TP Mazembe dhidi ya Simba SC.

Mechi hiyo ya robo fainali ya mkondo wa pili wa CAF CL, ambayo itapigwa leo mjini Lubumbashi, nchini DR Congo, huku kila mmoja akiwa na lengo kupata matokeo chanya ili watinge nusu fainali ya michuano hiyo.

Simba inahitaji ushindi ama sare yoyote ya mabao, ambayo itamwezesha kutinga hatua inayofuata ya nusu fainali ya CAF CL mwaka huu.

Wiki moja iliyopita miamba hiyo ilitoshana nguvu katika Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, jambo ambalo linawafanya Simba kuingia kwenye mechi hiyo wakiwa na malengo mawili.

Simba wanalazimika kuvuja jasho na damu ili kusonga mbele jambo ambalo si rahisi mbele ya mlima wa TP Mazembe wanapokuwa nyumbani.

Mabingwa hao mara tano wa michuano hiyo, hadi sasa wamecheza michezo minne ya CAF CL katika uwanja wao nyumbani msimu huu na hawajapoteza wala kufungwa, huku wakifunga mabao 13.

Ni pambano la aina yake kutokana na maandalizi ya vikosi vyote viwili kuelekea mchezo wa leo, kila upande umekuwa ukitoa tambo na kujinasibu kuibuka na ushindi japo dakika 90 tu ndio zitakata mzizi wa fitina.

Wakati Mazembe wakiamini watatumia vema uwanja wao wa nyumbani, Simba wanaingia na mchecheto wa kutofanya vizuri katika michezo ya ugenini msimu huu.

Katika michezo mitano Simba waliocheza ugenini ni mechi moja tu walishinda katika hatua za awali, huku wakipoteza minne ikiwemo michezo mitatu ya hatua ya makundi waliyobugizwa mabao 12.

Zahama lilianzia hukohuko Congo mjini Kinshasa walipopolewa 5-0 dhidi ya AS Vita Club, wakakubali kichapo kama hicho kule Miri mbele ya miamba ya Afrika Al Ahly kisha kubandikwa mabao 2-0 kule Algeria na JS Saoura.

Licha ya kupoteza mapambano hayo, kikosi hicho cha Kocha Patricck Aussems hakikuweza kufunga hata bao moja katika michezo hiyo ya ugenini.

Kesho Simba wanahitaji kuwa timamu kiafya, kiakili, kifikra, kihisia, na kisaikolojia kwa kusahau yaliyopita na kuuona mchezo wa kesho kuwa unamahitaji tofauti ili waweze kupata chochote.

Lakini Simba wanajambo la kuwashangaza wale wanaodhani nhawawezi kutoka salama katika pambano la kesho kutokana na maandalizi waliyoyafanya, aina ya mikakati walioingia nayo katika mtanange huo.

Aussems anahitaji kuingia kwenye mtanange wa kesho akiwa na wanajeshi watakao tekeleza maagizo yake kwa asilimia 100 ili kuweza kupambana na Mamba wa Lubumbashi ndani ya dakika 90.

Hata hivyo wawakilishi hao wa nchi wametua leo mchana jijini Lubumbashi na ndege ya kukodi na kufika salama mjini humo na kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mtanange huo unaotarajiwa kupigwa majira ya saa 10 jioni.

Mazingira ya mchezo yanawalazimu Simba kutumia vema kila nafasi itakayo jitokeza katika kandanda la leo kwani hakuna namna wanahitaji kupata mabao ili kujua hatma yao.

Kikosi cha wachezaji 18 kilichotua Lubumbashi kuwakabili Mazembe ni pamoja na Aishi Manula, Deogratius Munish, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein, Paul Bukaba, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, James Kotei, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, Clatous Chama, Rashid Juma, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco.

Kuelekea mchezo huo, Ofisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara aliandika jana kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa kuwa hawajaenda Congo kutalii bali wamekwenda kupambania klabu na taifa kwa ujumla jambo linaloongeza hamasa katika mpambano huo.
Mnara amesema hawaogopi lolote kwa wapinzani wao ila wanawapa heshima kwa  mafanikio na ukubwa wao katika medani za soka la Afrika wakiwa machampion mara tano wa mashindano hayo.
"Jasho na damu Lubumbash! Tunakwenda kibingwa tukiwa hatuna la kupoteza ila tunawaahidi jasho jingi litamwagika kupigania Simba na Nchi. Hatuogopi lolote kwa Mazembe pamoja na kuwapa heshima yao, " ameandika Manara.

No comments:

Post a Comment

Pages