Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na waandishi wa habari Jijini
Dodoma kuhusu Ukaguzi wa Maduka ya kubadilisha Fedha za Kigeni ambapo alisema lengo
lake sio kufuta biashara ya maduka hayo bali ni kudhibiti ukiukwaji washeria
uliokithiri na utakasishaji wa Fedha haramu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga,
akieleza kuwa jumla ya maduka 87 yamefanyiwa ukaguzi Jijini Dar es Salaam na ni
maduka matano pekee ndio yamebainika kutokiuka sheria, wakati wa mkutano kati
ya Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), na waandishi wa habari katika ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa
Habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango
Bw. Benny Mwaipaja (kushoto), wakiwa katika Mkutano na Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), ambapo Waziri huyo alisema hakuna mmliki wa
Duka la Kubadilisha Fedha ambaye amewasilisha malalamiko yoyote kwa
mamlaka husika
kuhusu zoezi la ukaguzi wa maduka hayo.
Mwandishi wa Habari wa
Gazeti la Mwananchi, Sharon Sauwa, akiuliza swali kuhusu kufungwa kwa maduka ya
kubadilisha fedha za kigeni wakati wa Mkutano kati ya waandishi wa habari
na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani) kuhusu ukaguzi wa maduka ya
kubadilisha fedha za kigeni, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akifafanua jambo wakati wa mkutano kati yake
na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dodoma. Kulia ni Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, na kushoto ni Kaimu Naibu
Katibu Mkuu na Kamishna wa Sera wa Wizara hiyo Bw.
Mgonya
Benedicto .
Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika
ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule,
Wizara ya Fedha na Mipango).
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UKAGUZI WA MADUKA YA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI
Dodoma, 1 Aprili, 2019: Katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha
kuwa Sekta ya Fedha inachangia ipasavyo utulivu na ukuaji wa uchumi nchini,
Benki Kuu ya Tanzania ilibaini uwepo wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo
yalikuwa yakiendeshwa pasipo kuzingatia Sheria ya Foreign Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho
ya mwaka 2017 na Taratibu za utoaji wa huduma za ubadilishaji wa fedha za
kigeni. Kufuatia hali hiyo, zoezi maalum la ukaguzi wa kina kwa maduka hayo lilifanyika
Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es Salaam siku ya tarehe 27 Februari 2019, 1 na 8
Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo vya Dola na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na
uvunjaji wa Sheria.
Zoezi hili limebaini pia uondoshwaji wa fedha katika mfumo
rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye mifumo ya utakasishaji wa fedha haramu,
kupokea Amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za
biashara husika, kudhoofisha thamani ya shilingi, pamoja na mambo mengine ambayo
yalianza kuathiri usalama wa nchi kwa ujumla. Kwa mfano, baadhi ya maduka yaligundulika
kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni lakini fedha kidogo za
kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya fedha za kigeni zilizobaki.
Ni vizuri ieleweke kuwa, zoezi la ukaguzi wa maduka ya kubadilisha
fedha za kigeni lilitekelezwa kwa kuzingatia Sheria za nchi tofauti na
malalamiko na tuhuma mbalimbali zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa Sheria
na haki kwa wamiliki wa maduka hayo. Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna
mmiliki yeyote wa duka aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye
mamlaka husika. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka nyingine za
Serikali zinafuatilia kwa umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo
zinazotolewa.
Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza majukumu yake kwa
umakini. Hivyo, Serikali inauthibitishia umma wa Watanzania kuwa katika zoezi
la ukaguzi wa Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni hakuna fedha au mali yeyote
iliyotaifishwa. Taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa kuchukua vielelezo mbalimbali
zikiwemo fedha, kompyuta, simu za viganjani, mashine maalum za kuhifadhi
taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia uchunguzi. Aidha, lengo la zoezi
hili sio kufuta biashara ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa watu
binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa sheria uliokithiri, ukwepaji wa kodi na
utakatishaji wa fedha haramu. Maduka machache ya kubadilisha fedha za kigeni
ambayo yalizingatia Sheria na Kanuni za Foreign
Exchange na masharti ya biashara hiyo yaliachwa kuendelea na utoaji wa
huduma hiyo.
Hivi sasa Serikali imeandaa Kanuni mpya kwa ajili ya biashara
ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba
leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi yeyote na
masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.
Kanuni hizo zinalenga kuweka mazingira mazuri ya biashara
ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi jumla, na inakuwa yenye
manufaa kwa nchi. Kwa kuzingatia maduka mengi yaliyokaguliwa yamefungwa, Benki
Kuu ya Tanzania imechukua tahadhari ya kuhakikisha huduma ya ubadilishaji fedha
za kigeni inaendelea nchini kwa kutolewa na benki zote pamoja na Shirika la
Posta. Benki Kuu ya Tanzania itakuwa inatoa taarifa kuhusu upatikanaji wa
huduma hiyo na kuzihimiza benki za biashara na Shirika la Posta kutoa taarifa
kwa umma kuhusiana na huduma katika maduka yaliyofunguliwa na benki hizo na
Ofisi ya Posta.
Kwa kipindi kifupi cha utekelezaji wa zoezi la udhibiti wa
biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, thamani ya shilingi imeimarika na
upatikanaji wa fedha za kigeni katika benki za biashara umekuwa mzuri. Kabla ya
zoezi la udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha ya kigeni dola ya Marekani ilikuwa
inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,450 na baada ya utekelezaji wa zoezi hivi
sasa dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa shilingi 2,300. Aidha, Benki za
biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya jumla ya dola za Marekani milioni 15
kwa siku. Ni matarajio ya Serikali kuwa udhibiti huu utaziwezesha Benki za
biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za kigeni kwa wingi kwenye soko la
fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Serikali inatoa tahadhari kwa wananchi kutoshiriki kwenye
biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia zisizo halali. Hivi sasa kuna
taarifa kwa baadhi ya maeneo ya mipakani na majiji ya Dar es Salaam na Arusha
wamejitokeza watu wanaofanya biashara haramu ya kubadilisha fedha za kigeni
ambao wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi. Vyombo vya usalama ikiwemo jeshi
la polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha biashara hii haramu (Black
Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba wamekamatwa na kufikishwa
mahakamani.
Serikali inapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa inayo
akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo dola za Marekani bilioni 4.67 hadi
tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi
kwa kipindi kisicho pungua miezi 4.8. Hivyo, wasiwasi kuwa Serikali imechukua
hatua ya kufunga baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwa sababu
haina akiba ya fedha za kigeni si ya kweli hata kidogo. Aidha, hofu kwamba nchi
inarejea katika kipindi cha nyuma ambapo fedha za kigeni zilikuwa zinatolewa
kwa vibali (rationing) ili kukidhi mahitaji ya fedha hizo kwenye utekelezaji wa
miradi mikubwa ya maendeleo, nazo hazina msingi.
Mapato ya Nchi yanayotokana na vyanzo vya fedha za kigeni
kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi yalikuwa na thamani ya dola za Marekani
milioni 8,554.5 kwa mwaka unaishia Februari 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.4
ikilinganishwa na fedha za kigeni zilizopatika mwaka unaishia Februari 2018. Ongezeko
hilo la mapato ya fedha za kigeni kwa Nchi yamechangiwa zaidi na uuzaji wa
bidhaa zisizo asilia nje ya nchi zikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni
3,878.5 sawa na asilimia 10.3 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Vile vile,
huduma zilizotolewa nje ya nchi kama vile usafiri na usafirishaji na utalii
ziliingiza jumla ya dola za Marekani milioni 4,074.1 sawa na ongezeko la
asilimia 6.1 ikilinganishwa kiasi kilichopatikana mwaka ulitangulia.
Aidha, Serikali
inachukua fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha
kutosha ambacho kina utoshelevu wa asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19.
Hivyo, Serikali haitarajii kutumia fedha za kigeni kuagiza chakula kutoka nje ya
nchi isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya katika siku zijazo.
Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania, inawataka
wafanyabiashara ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kuzingatia na kutii
Sheria ya Foreign Exchange 1992,
Kanuni ya Foreign Exchange (Bureau de
Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017, Masharti ya biashara
ya huduma ya kubadilisha fedha za kigeni na Maelekezo ya Msimamizi (BOT) wa
Sekta ya Fedha Nchi. Mwisho Serikali inawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuwa
waelewa na watulivu wakati wote zoezi la ukaguzi likiendelea, licha ya
kujitokeza kwa taarifa za upotoshwaji wa zoezi hili.
IMETOLEWA NA:
DKT. PHILIP ISDOR
MPANGO
WAZIRI YA FEDHA NA
MIPANGO
No comments:
Post a Comment