Na Farida Ramadhani na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imeleeza kuwa imeshawalipa
Wazabuni 2048 kiasi cha Shilingi 199 tangu kutolewa kwa tamko la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 3
Januari, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam la kutaka Wazabuni wote wanaoidai
Serikali walipwe.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa (CCM), Mhe. Ritta
Kabati, aliyetaka kujua baada ya tamko la Mhe. Rais kuhusu Wazabuni wote
wanaoidai Serikali walipwe ni Wazabuni wangapi wameshalipwa.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alieleza kuwa kati ya Wazabuni 2048 waliolipwa na Serikali, Wazabuni 1,277
walihudumia Sekretarieti za Mikoa na 771 walihudumia Wizara, Taasisi na Wakala
za Serikali.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa Shilingi
3,729,605,175 zimetumika kulipa Wazabuni waliotoa huduma kwa Sektretarieti za
Mikoa na Shilingi 195,334,409,791.64 zimetumika kulipa Wazabuni wa Wizara,
Taasisi na Wakala za Serikali.
“Ikumbukwe kuwa madeni yote
haya yalilipwa baada ya uhakiki kufanyika”, alisisitiza Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea
kulipa madai mbalibmali ya wazabuni kulingana na upatikanaji wa fedha, sambamba
na uhakika wa madai husika.
Dkt. Kijaji amesema kuwa ili kukamilisha zoezi la uhakiki kwa wakati, wazabuni
wote wanatakiwa kutoa ushirkiano, hususan kuwasilisha taarifa na vielelezo
sahihi vya madai yao pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
Katika swali la nyongeza Mbunge wa
Viti Maalum Mhe. Kabati alitaka kujua vigezo vilivyotumika kuwalipa wazabuni
hao.
Akijibu swali hilo la nyongeza Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa vipo vigezo
vingi ambavyo Serikali imevitumia kulipa madeni hayo moja ikiwa umri wa deni,
madeni ambayo yamekaa kwa muda mrefu na ambayo tayari yamehakikiwa ndiyo
yanapewa kipaumbele katika malipo.
Aliongeza kuwa kigezo cha pili ni
riba Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa madeni ambayo riba yake inakuwa
kulingana na muda, ili Serikali isiendelee kuumia wala mwananchi asiendelee
kuumia.
No comments:
Post a Comment