Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Serikali
imesema haitasita kuwachukulia hatua watu wanaowanyanyasa watoto kwa kukiuka
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Hayo
yamesemwa leo, Bungeni Jijini Dodoma na
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Josephat Kandege alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mgebi
Jadi Kadika juu ya mikakati ya Serikali ya kuondoa tatizo la kuwakosesha watoto
haki za msingi na malezi bora kwa kuwatumia katika kutoa huduma ya kubeba
mizigo na kupewa ujira mdogo.
"Huduma
za ulinzi wa mtoto zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na
Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa Fedha 2017/18 hadi 2021/22,"
amesema Kandege.
Ameendelea
kusema, tathmini imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba
mizigo masokoni ni matokeo ya umaskini uliokithiri kwa baadhi ya Kaya,
kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na ukatili
dhidi ya watoto.
Amesema,
mkakati unaotekelezwa na Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za
msingi za mtoto kupata elimu na malezi bora. Aidha, utoaji wa elimu msingi bila
malipo umetoa fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa
kuanza elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi.
Aidha
ametoa wito kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea, kuwatunza na kuwalinda
watoto ambao ni Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo
haziendani na umri wao.
No comments:
Post a Comment