Na Ismail Ngayonga, MAELEZO
Mkakati
wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) ambao ni mwongozo
muhimu katika kuleta maendeleo endelevu, unatambua kuwa mazingira bora ni
msingi wa maendeleo endelevu na kupunguza umaskini.
Mkakati
huu umeainisha malengo 15 yanayohusu mazingira na utekelezaji wa MKUKUTA
unahusisha wadau mbalimbali, ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR) inalo jukumu
la kuratibu ujumuishaji wa masuala ya mazingira katika mipango na bajeti za
kisekta za kupunguza umaskini.
Katika
kutekeleza jukumu hili, OMR imefanikisha na inaendelea kutekeleza mipango na
programu kadhaa ikiwemo ile ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira,
Sheria ya Mazingira na Kanuni zake.
Sheria
ya Mazingira ya mwaka 2004 imeeleza wazi wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali
kuanzia serikali za mitaa hadi taifa ikisisitiza mipango na usimamizi wa
matumizi endelevu ya mazingira: kudhibiti uchafuzi wa mazingira; utunzaji wa
taarifa na takwimu za mazingira; utafiti na ushiriki wa jamii na utekelezaji wa
majukumu yatokanayo na mikataba ya kimataifa.
Akiwasilisha
Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Nchi
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba anasema Serikali
kupitia Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
limeendelea kutekeleza Ajenda ya Taifa ya Utafiti katika Mazingira (NERA
2017-2022).
Waziri
Makamba anasema katika mwaka wa fedha 2017/18, NEMC kwa kushirikiana na wataalam
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamisheni ya Matumizi ya Ardhi, Taasisi ya
Huduma za Misitu na Halmashauri ya Wilaya ya Same imefanya tathmini ya hali ya
mazingira kwenye maporomoko ya ardhi
katika milima ya Mamba Miamba iliyopo Wilayani Same.
Anaongeza kuwa katika tathmini ya utafiti huo ilibaini
chanzo cha maporomoko hayo ni aina ya udongo wa mfinyanzi uliopo katika eneo
hilo pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika huko ikiwa ni pamoja na
ukataji holela wa miti na uchomaji moto hovyo katika maeneo hayo.
Aidha
anasema NEMC limepeleka mapendekezo ya kuzuia uharibifu wa
mazingira katika eneo hili kwa wadau ili hatua thabiti za uhifadhi zichukuliwe,
ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kulitangaza eneo hilo kuwa ni eneo
tete la mazingira na kulitengenezea mpango wa kudhibiti uharibifu wa mazingira.
“Katika mwaka 2017/18, Baraza limefanya utafiti wa
uharibifu wa mazingira wa Bwawa la Mindu
lililopo katika Manispaa ya Morogoro na mmonyonyoko wa ardhi katika
fukwe za Ziwa Viktoria. Matokeo ya tafiti hizo yalibainisha vyanzo
mbalimbali vya uharibifu na kupendekeza hatua za kuchukuliwa” anasema Waziri
Makamba.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba anasema NEMC imefanya
utafiti wa namna ya kuboresha mazingira ya mji wa Dodoma ili uwe ‘mji wa
kijani’ kwa kutumia dhana za green
city, eco-buildings na sustainable construction.
Akifafanua zaidi anasema katika mwaka 2017/18, Baraza
limeendelea kuratibu shughuli za Hifadhi Hai kwa kuwasilisha taarifa za awali katika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa ajili
ya kuingiza Hifadhi ya Gombe Ugalla -Masito kwenye mtandao wa Hifadhi Hai za
Dunia.
Waziri Makamba anasema NEMC pia imeandaa Mpango wa
Usimamizi wa Mazingira (Environmental
Management Plan-EMP) kwa maeneo mawili ambayo ni Dakio la Bonde la Kihansi
na eneo la Ziwa Chala–Jipe. Aidha, Baraza limekamilisha zoezi la uwekaji mipaka
katika eneo la Kihansi ambalo linatarajiwa kutangazwa kuwa eneo lindwa la
kimazingira.
Anasema katika mwaka 2018/19, Baraza litaendelea
kukusanya takwimu na na kuandaa taarifa za hali ya mazingira ya milima nchini, taarifa
ya mazingira ya pwani (State of the
Coastal Environment Report – SOCR, 2018); utafiti wa mifumo ya ikolojia ya
hali ya mabonde ya mito mikubwa, maeneo ya malisho ya mifugo na wanyamapori.
Tanzania
ni nchi yenye uwezo mkubwa wa kuweza kutoa manufaa kimazingira duniani, kwa
kuzingatia changamoto za kimazingira za kitaifa na kimataifa zinazoikumba nchi
ni wajibu wa wadau wa kitaifa na kimataifa kuwekeza rasilimali ili kukuza,
kuchangia na kuthibiti maliasili ili kuboresha na kuongeza mchango wa Tanzania
katika mazingira Duniani.
No comments:
Post a Comment