HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2019

KILICHOMKWAMISHA IBRAHIMU AJIBU KUTUA TP MAZEMBE HIKI HAPA


 Ajibu.



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


WEKUNDU wa Msimbazi wamefanikiwa kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), lakini gumzo katika viunga vya soka nchini sio taji hilo la 20 la Simba, bali mshambuliaji anayemaliza muda wake Yanga, Ibrahimu Ajibu Migomba ‘Ibra Cadabra.’


Wakati msimu wa TPL 2018/19 ukitarajia kufikia ukomo kesho, Ajibu ameteka vijiwe vyote vya soka, baada ya kuripotiwa kukataa ofa ya kujiunga kama mchezaji huru katika kikosi cha TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Uamuzi wa Ajibu kuitolea nje TP Mazembe, umegubika sio tu ubingwa wa Simba katika TPL, bali pia gumzo la ‘utani wa jadi’ la wachezaji wa Simba kuomba viatu, jezi na vitu vingine kwa wachezaji wa Sevilla, mwishoni mwa pambano lao la kirafiki la kimataifa.


Simba walikuwa wenyeji wa Sevilla ya Hispania, katika pambano la kirafiki lililopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambako Simba walikubali kipigo ‘cha usiku’ cha mabao 5-4, kabla ya Adam Salamba kuongoza tukio la ‘fair play’ la kuomba viatu kwa Ever Banega.


Sasa unaambiwa taji la TPL lililotwaliwa na Simba pamoja na matukio yote yaliyoambatana na mechi ya Sevilla (ikiwemo matokeo na fair play zote), vimegubikwa na uamuzi wa Ajibu kudaiwa kuigomea ofa ya TP Mazembe, ili atimize ndoto za kurejea Msimbazi. Habari Mseto inayo mkanda mzima, ambao uko hivi.


Sababu kuu ya TP Mazembe kushindwana na Ibrahim Ajibu ni klabu ya Simba, kwa sababu TP Mazembe walituma barua Yanga (Mei 16 yenye Kumbukumbu Namba: 008/MKC/TPM/2019) ya kuomba kumsajili Ajibu kama mchezaji huru, pindi atakapomaliza mkataba wake

Mei 23 TP Mazembe waliiomba Yanga wamruhusu Ajibu afanye mazungumzo kuhusu usajili huo.


Kabla ya Mei 23, Meneja wa Ajibu aliwasiliana na klabu ya Simba kuwaaomba wamruhusu Ajibu ajiunge na TP Mazembe (kwa sababu alikuwa amesaini mkataba wa awali na klabu hiyo), ambako alikuwa akisubiri kumaliza msimu na Yanga ili amalizane rasmi na Wekundu wa Msimbazi.


Baada ya Meneja huyo kuwaomba Simba wamruhusu Ajibu kutua TP Mazembe, ndipo klabu ya Simba ikawaambia TP Mazembe waje kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu wao wana mkataba wa awali na Ajibu na alishachukua sehemu ya fedha za usajili (inaaminika ni Sh. Mil. 80).


Hayo yote yalikuwa yakijiri wakati ambapo tayati TP Mazembe wameshaweka mezani ofa ya dola 30,000 ya kumlipa Ajibu kama mchezaji huru ili kujiunga na kikosi chao, sambamba na mshahahara wa dola 3,000 kwa mwezi (ofa ambazo zilikosa thamani kwa Ajibu, kisa mkataba wa awali Simba).


Simba wakawambia TP Mazembe kuwa Ajibu anauzwa dola 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh. Mil. 220 za Kitanzania na kuwapa sharti la kuweka kwenye mkataba wake kipengele kitakachowapatia asilimia 20 ya mauzo yake, iwapo atauzwa kutoka Mazembe kwenda kwingineko.


Ndipo TP Mazembe ikasitisha mpango wa kumsajili kwa sababu yenyewe ilikuwa inajua Ajibu ni mchezaji huru, ambapo sasa wakaandika barua kwa uongzoi wa Yanga, kuelezea kusitishwa kwa mchakato wao uliowasukuma kuandika barua ya awali Mei 16.


Sasa unaambiwa gumzo mitandaoni na vijiweni ni kukwama kwa mchakato huo, wengi miongoni mwa mashabiki wakimtupia lawama Ajibu, kutokana na kilichomo katika barua ya pili ya Mazembe, inayosema ‘wamesitisha jaribio lao baada ya kutoafikiana matakwa binafsi na Ajibu.’

No comments:

Post a Comment

Pages