MCHUNGAJI wa Kanisa la GRC, Ubungo jijini Dar es Salaam Anthony
Lusekelo amesema kuwa Taifa halihitaji kiongozi anayetokana na udini bali
anayenadi sera.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mchungaji Lusekelo (pichani), alisema
baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotumia nyumba za ibada kujinadi ni ishara ya
kupoteza mvuto kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa Kiroho alisema, Taifa linahitaji kupata mgombea
ambaye ananadi sera zake ambazo zitakubalika na wananchi na sio kutumia nyumba
za ibada kutafuta kura.
“Hili Taifa halina dini na wala halihitaji mgombea anayetokana na
dini fulani bali aliye na sera zinazokubalika ukiona mgombea anatumia nyumba za
ibada kutafuta kura huyo hana nguvu za kisiasa,” alisema.
HAMAHAMA
Mchungaji Lusekelo alionyesha kuchukizwa na baadhi ya viongozi
wanaohama hama vyama vya siasa na kusema kuwa hatua hiyo inapoteza uaminifu kwa
wananchi waliowachagua.
Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa
wakihama vyama hivyo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatua
inayosababisha kurudi katika uchaguzi mdogo.
, siasa sio uadui lakini kitendo cha baadhi ya viongozi kushindwa
kusimamia kauli zao na kuamua kujiondoa katika vyama vyao vinapoteza uaminifu.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanatumia vyama vyao na
kuyasimamia yale wanayoyaahidi kwa wananchi kwa kuhimiza umoja, mshikamano na
uzalendo.
“Kuhamahama sio shida lakini kwangu mimi nachukizwa na vitendo
hivyo kwani inaonyesha wazi viongozi hao hawawezi kuyasimamia yale
wanayoyaahidi,” alisema.
UCHAGUZI
Mchungaji Lusekelo alisema, kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa
hauna tija ni kutaka kuihamsha na kulisumbua Taifa.
Alisema kuwa kuna sherehe nyingi Rais John Magufuli ameweza
kuzifuta hivyo kama angeweza kumshauri kiongozi huyo uchaguzi huo ungesogezwa
na kufanyika mwakani 2020 ili kupunguza gharama.
“Kama ningekuwa Waziri Mkuu au Waziri wa Tamisemi ningeshauri na
kumuomba Rais awaache viongozi waliopo madarakani wa serikali za mitaa
wakaendelea wao na uchaguzi tukaufanya mwaka 2020,” alisema.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema, hatua hiyo itaweza kulifanya
Taifa likaendelea kupumua na viongozi wakaendelea kusaidia kufikia maendeleo ya
uhakika.
Kumkosoa Rais
Alisema kuwa sio maadili kumkosoa kiongozi wa nchi kihuni na
kuwataka wale wanaokosoa kusubiri kiongozi huyo atakapoondoka madarakani
watumie fursa hiyo kumkosoa.
Aliwataka wanaohitaji kukosoa kuwaachia wabunge ambao wanaweza
kutumia muhimili huo kukosoa kwa weledi.
No comments:
Post a Comment