Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba (waliokaa kulia) na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Mfuko wa Fidia kwa Wfanyakazi kutoka Zambia,(WCFCB), Dkt. Elizabeth Lungu Nkumbula, wakitia saini makubaliano ya ushirikiano baina ya mifuko hiyo, katika hafla iliyofanyika ofisi za WCF Dodoma Jumatatu Mei 27, 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba (kulia) na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kutoka Zambia, (WCFCB) Dkt. Elizabeth Lungu Nkumbula, wakibadilishana hati baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano baina ya mifuko hiyo. Hafla hiyo iliyofanyika ofisi za WCF Dodoma Jumatatu Mei 27, 2019.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TANZANIA na Zambia kupitia
Mifuko ya Fidia kwa Wafanyakazi, wamesaini mkataba wa ushirikiano utakaosaidia
kubadilishana uzoefu kati ya mifuko hiyo.
Akizungumza mara baada ya
kutiliana saini mkataba huo, kwenye ofisi za WCF jijini Dodoma Jumatatu Mei 27,
2019, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha
Mshomba alisema, Zambia inauzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika sekta ya hifadhi
ya jamii katika kulipa mafao ya Fidia kwa Wfanyakazi kwa hivyo makubaliano hayo
yana manufaa makubwa.
Alisema makubaliano hayo ni ya
kawaida kati ya mifuko na kwamba WCF na WCFCB watabadilishana uzoefu katika
masuala ya namna ya ulipaji mafao, namna ya kuzuia ajali na magonjwa kazini kwa
sababu mambo hayo ni muhimu sana katika mifuko ya fidia.
“Nguvu kazi ya taifa
inapolindwa tija huongezeka makazini na jambo hili hudhihirika pale pato la
taifa linaongezeka hususan kwetu sisi ambao tunajenga uchumi wa viwanda jambo
hilo ni muhimu sana.”Alisema Bw. Mshomba.
Alisema kwa uzoefu ambao Zambia
watakuwa wameupata kutoka kwao wataweza kuboresha huduma zao, na tayari Dkt.
Nkumbula amethibitisha kuwa serikali ya Zambia inautegemea Mfuko huo katika
kusaidia nguvu kazi ya taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Zambia (WCFCB), Dkt.
Elizabeth Lungu Nkumbula alisema, imekuwa ni siku njema kwao kwa kujenga
ushirikiano wa pamoja katika eneo la hifadhi ya jamii.
“Zambai na Tanzania chini ya
uongozi wa Dkt. Keneth Kaunda na Mwalimu Nyerere, waliweza kujenga reli ya
TAZARA na bomba la mafuta TAZAMA kwa hivyo ushirikiano huu wa leo ni kumbukumbu
ya ushirikiano uliojengwa kwa muda mrefu na viongozi hao wa mataifa hayo
mawili.” Alifafanua.
Alsema ushirikiano huu
utasaidia pande mbili kubadilishana uzoefu katika kutoa huduma za ulipaji fidia
na mbinu za kuzuia majanga yatokanayo na kazi na hivyo kusaidia mataifa hayo
kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment