HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 31, 2019

Serikali ya Marekani Yatoa Misaada Yenye Thamani ya Dola 750,000 Ili Kutengeneza Ajira Kwa Vijana wa Vijijini

Mwakilishi wa Tanzania Bora Initiative, Abella Bateyunga (kulia), akipokea mfano wa hundi ya Sh. Mil 209,057,674. Msaada huo unatolewa chini ya mradi wa Inua Vijana wa "Feed the Future Tanzania". Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas na Msimamizi wa Miradi ya Vijana Sekta Binafsi USAID, Joyce Mndambi. (Picha kwa Hisani ya Ubalozi wa Marekani).
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa wenye thamani ya dola 750, 000 kwa taasisi tisa mkoani Mbeya. (Picha kwa Hisani ya Ubalozi wa Marekani)

Mbeya, Tanzania

SERIKALI ya Marekani imetoa misaada yenye thamani ya dola 750,000 kwa taasisi tisa ambazo zinasaidia utengenezaji wa ajira, ujasiriamali, uongozi, na maisha bora kwa vijana. 

Misaada hiyo inatolewa na mradi wa Inua Vijana wa "Feed the Future Tanzania", inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na wanatarajia kutengeneza ajira 950 kwa vijana katika makampuni 700 mapya au ambayo yanaongozwa na vijana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, na Zanzibar. 

Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Andrew Karas, na Mheshimiwa Suleiman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), walikabidhi misaada hiyo kwa taasisi husika. 

Wakati wa hotuba yake, Bwana Karas alibainisha kuwa “Kuwekeza katika uongozi wa vijana nchini Tanzania ni kipaumbele cha USAID na Serikali ya Tanzania. 

Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana, na idadi ya wananchi wake inatarajiwa kuongezeka mara mbili ndani ya miaka 25 hadi 30 ijayo. Jitihada za makusudi zinahitajika kwa serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha kuwa nguvu, vipaji, na matumaini ya vijana wa leo, pamoja na kizazi kijacho, zinafanya Tanzania kuwa mahali pa mafanikio kwa wote.”

Mradi wa Inua Vijana unahamasisha vijana wa vijijini kushiriki katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuwapatia fursa za kiuchumi vijana wenye umri wa miaka 15-35 pamoja na kuhamasisha uongozi na mienendo ya kiafya. Kupitia misaada hii, Inua Vijana ya Feed the Future Tanzania itabadili changamoto kuwa fursa kwa vijana wa vijijini kuongoza na kushiriki katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages