Na
Frank Mvungi- MAELEZO
Thamani ya Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) imefikia Trilioni 5.8 hali inayoonesha kuwa mfuko huo
unaendelea kuimarika na hivyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama wake.
Akizungumza katika kipindi cha
‘TUNATEKELEZA’ Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Hosea Kashimba, amesema kuwa
kuunganishwa kwa mifuko ya GEPF, LAPF, PSPF na PPF kunatoa fursa ya kuimarisha zaidi sekta ya hifadhi ya
Jamii hali iliyochangia thamani ya mfuko mpya wa PSSSF kuendelea kukua hata
katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.
“Tumeshatumia zaidi ya Trilioni
moja kulipa mafao kwa wanachama wetu hali inaonesha kuwa mfuko upo katika hali
nzuri hivyo niwatoe hofu wanachama wetu kwani tumejipanga kuhakikisha
tunawahudumia vizuri kwa mujibu wa sheria na kanuni za hifadhi ya jamii “
Alisisitiza Kashimba.
Akifafanua Kashimba amesema kuwa, wastaafu elfu kumi wameshalipwa mafao yao
tangu kuanzishwa kwa mfuko huo na wachache ambao hawajalipwa ni wale ambao
hawajahakiki taarifa zao kwa muda
uliotolewa hivyo aliwataka kujitokeza na kuhakikiwa ili warejeshwe
katika daftari la malipo.
“Ukishahakikiwa tunakurejesha
kwenye daftari la malipo na utalipwa malipo yako yote ambayo hukuwa umelipwa
hapo awali kabla ya kuhakikiwa hivyo niwatoe hofu wanachama wetu na kuwataka
wajitokeze kuhakiki taarifa zao” Alisisitiza Kashimba.
Alieleza kuwa,takribani wastaafu
113,000 wamehakikiwa kati ya wastaafu 124,000 waliotakiwa kuhakikiwa hivyo kuwaomba wanachama wa mfuko
huo nchini kuendelea kujitokeza kuhakikiwa kupitia ofisi za mikoani kwa kuwa huduma zinazotolewa makao
makuu zinatolewa pia mikoani.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa
uchumi wa viwanda Bw. Kashimba amesema kuwa mfuko huo umejipanga kikamilifu
kuendelea kutekeleza dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali kulingana na miongozo
ya Serikali.
“Tumewekeza katika Kiwanda cha
viatu Karanga Moshi kwa ubia na Jeshi la Magereza na tunatarajia Kiwanda hiki kitatoa
ajira elfu nne na kuzalisha jozi milioni
1. 2 kwa mwaka, tunawekeza kwenye kiwanda cha kuchakata tangawizi kilichopo
Wilayani Same, Kiwanda cha nyama Morogoro na vingine kulingana na miongozo ya
uwekezaji na maagizo ya Serikali “Alisisitiza Kashimba.
Aidha, Mitambo ya kuzalisha viatu
katika kiwanda cha Karanga inatarajiwa
kuwasilisi nchini na kufungwa katika kiwanda hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu
ili kutekeleza azma ya sekta hiyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi
jumuishi kupitia viwanda.
Hata hivyo Kashimba aliwataka
wanachama wote kuhakikisha kuwa waajiri wanawasilisha michango yao kwa wakati
ili kuepuka usumbufu wakati wa kustaafu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa Uendeshaji wa mfuko huo Bw. Victor Kikoti amesema kuwa baadhi ya mafao
yanayotolewa ni yale ya muda mfupi na muda mrefu lengo likiwa kuwawezesha
wanachama wote kuishi maisha bora hata baada ya kustaafu.
“Wanachama wetu wataendelea
kunufaika na huduma zetu na hata pale inapotokea bahati mbaya mwanachama wetu
amefariki basi haki zake hazitapotea na zinalindwa kwa mujibu wa sheria ili
ziwanufaishe warithi wake” Alisisitiza Kikoti.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Bw. Gilbert Chale amesema kuwa mfuko huo
umejenga mifumo bora inayounganisha Ofisi zote na makao makuu ya mfuko ili
kuimarisha huduma na tija kwa wanachama.
Kuunganishwa kwa mifuko ya Hifadhi
ya Jamii ya PSSSF, GEPF, LAPF na PSPF kumewezesha kuanza rasmi kwa mfuko mpya
wa Hifadhi ya Jamii katika Utumishi wa Umma (PSSSF) mwaka 2018.
No comments:
Post a Comment