*Wajishindia dola za Marekani 5,000 na
3,000 kila mmoja
VIJANA wawili
wa Kitanzania, Zakaria Sheha Ally na Shamsi Mwalimu Said wamechukua nafasi ya
kwanza na ya tatu kwenye fainali za 27 za tuzo ya kimataifa ya kuhifadhi Quran
tukufu.
Zakaria
Sheha Ally (16) kutoka Tanzania Bara na Shamsi Mwalimu Said (19) kutoka
Zanzibar wameibuka na kitita cha dola za Marekani 5,000 na dola 3,000 kila
mmoja baada ya kuwashinda wenzao nane waliofanikiwa kuingia fainali hizo ambao
walitoka Afrika Kusini, Sudan, Malaysia, Uturuki, Yemen, Kenya, Burundi na Uingereza.
Nafasi ya
pili imechukuliwa na kijana Gaffari Mohammed (14) kutoka Uingereza ambaye ameibuka
na kitita cha dola za Marekani 4,000. Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya
ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, mwaka huu yalishirikisha vijana 10 kutoka nchi 10
duniani.
Tuzo hizo
zimetolewa leo (Jumapili, Mei 26, 2019) wakati wa kilele cha mashindano ya 27
ya Kimataifa ya Kuhifadhi na Kusoma Qur’an tukufu na utoaji tuzo yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na mamia ya waumini wa Kiislamu waliofurika kushuhudia kilele cha Tuzo ya
Kimataifa ya Quran iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran nchini, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuhifadhisha
Quran kunapaswa kuwa msingi imara katika kujenga jamii bora.
“Tuendelee
kuhimiza suala la malezi bora ya vijana wetu kwa lengo la kuwafanya wawe raia
wema, wakweli, wazalendo na wenye manufaa kwa nchi yao. Quran inatusisitizia
sana kuhusu suala la uadilifu. Kwa mfano, katika Quran 9:119, Mwenyezi Mungu
Mtukufu anatukumbusha waumini kumuogopa Mungu na kuambatana na wale walio
wakweli wa maneno na vitendo,” amesema Waziri Mkuu.
Amewataka wazazi
wa Kiislamu wahakikishe wanawasimamia vema watoto wao na kuwahifadhisha Quran badala
ya kutoa msukumo pekee kwenye elimu ya kimazingira. “Sote ni mashahidi kwamba
vijana wetu wanao uwezo wa kuhifadhi Quran na wakati huohuo wakasoma na
kuhitimu fani mbalimbali katika elimu ya mazingira.”
“Tukumbuke
kwamba mafanikio ya duniani na akhera hayapatikani kwingine isipokuwa ni kupitia
Quran. Hivyo basi, tuwafunze Quran vijana wetu ili waweze kukabiliana na
changamoto nyingi zinazoibuka kwenye ulimwengu wa sasa hususan suala zima la mmomonyoko
mkubwa wa maadili,” amesisitiza.
Amesema njia
mojawapo ya kuwasaidia vijana kukabiliana na hali ya sasa ya dunia ya
utandawazi ni kuwasomesha na kuwahifadhisha Quran. “Vijana waliosoma na
kuihifadhi Quran ni vigumu kuenenda kinyume na maadili kwani Quran ndiyo njia
pekee ya kuwachunga na kuwafanya waonyeke dhidi ya vitendo vinavyokwenda
kinyume na uadilifu.”
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran nchini kwa kuendelea
kuwapatia vijana wa Kitanzania mwongozo na msingi wa maisha yao kupitia Quran
kwani kwa kufanya hivyo wanakuwa wanawaongezea vijana hao uelewa sahihi wa dini
yao na elimu ya kutosha ya mazingira (yaani circular education).
“Kwa kufanya hivyo, Jumuiya inalipatia
Taifa la Tanzania nguvu kazi yenye uadilifu mkubwa katika utekelezaji wa
majukumu yake sambamba na uwezo na kujiamini katika kuisoma na kuihifadhi Quran
tukufu,” amesema.
Amewakumbusha viongozi wa taasisi
hiyo watenge muda maalum wa mashindano hayo kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa,
kanda, kitaifa ndipo wawagawe kwenye makundi mawili makubwa. “Mkitoka hapo washindanishwe
kwa bara la Afrika na kisha mashindano ya dunia. Siyo mnamaliza mashindano ya kimataifa
halafu unasikia kuna mashindano ya wilaya au mkoa,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Mufti wa Tanzania,
Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali alisema tuzo za leo zimethibitisha kuwa kusoma
elimu ya mazingira hakuharibu elimu ya dini. “Iwe changamoto kwa Waislamu kwamba
msingi wa elimu ya dini hauchafui elimu ya dini, kwani kuna watu hawataki
kusoma elimu ya mazingira kwa kisingizio kuwa mtume hakusoma, sasa mtume
atasoma kila kitu?” alihoji.
“Mambo ya uchumi,
kijamii, sheria na ufundi yalielezwa na Mtume Muhammad (S.A.W) na Quran imeyazungumzia
sana. Kusoma elimu ya mazingira ni muhimu kwa sababu zipo pia aya zaidi ya 70 katika
Quran tukufu ambazo zinaelezea mambo hayo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, Sheikh
Othman Ali Kaporo alisema walilazimika kuanzisha taasisi ili kuwafundisha
vijana maadili mema kwani miaka ya 80 - 90 ilikuwa shida kumpata kijana mwenye
uwezo wa kuhifadhi hata juzuu tatu tu.
“Hivi sasa
taasisi yetu ina vijana zaidi ya 1,000 katika sekta tofauti lakini hakuna hata
mmoja aliyekutwa katika mambo ya dawa za kulevya, ufisadi au mambo ya hovyo.
Quran ni kinga. Quran ndiyo mafanikio, na kwa malengo hayo, ndiyo maana tunafanya
mashindano haya,” alisema.
No comments:
Post a Comment