HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2019

VUMBI LA KUFUNGA MSIMU LIGI KUU TANZANIA, NANI KULIA, NANI KUCHEKA?

Dar es Salaam, Tanzania

MSIMU wa soka wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL 2018/19), unakamilishwa Jumanne ya Mei 28, ambako timu zote 20 za ligi hiyo isiyo na mdhamini mkuu, zitajitupa viwanjani kusaka ushindi muhimu, zaidi ya nuzu ya timu hizo zikipigana vita ya kutoshuka daraja.

Tayari Wekundu wa Msimbazi Simba wameshatazwa mabingwa kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kufikisha pointi 92, ambazo haziwezi kufikiwa na mahasimu wao Yanga, waliokuwa wakiongoza ligi hiyo kwa muda mrefu, huku Simba wakiwa na viporo kibao.

Simba wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, kuwavaa Mtibwa Sugar, katika pambano litalotumika kuwakabidhi taji, mchakato uliokwama katika pambano lililopita dhidi ya Biashara United ya Mara, kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wa wahusika.

Mtibwa ni kama hawana cha kupoteza, kwani pointi zao 49 kunako nafasi ya tano ya msimamo, zinawapa uhakika wa kubaki TPL kuelekea msimu wa 2019/20, hivyo haitarajiwi ushindani mkali baina yao, badala yake zitakuwa katika vita ya kulinda heshima tu.

Baada ya kutambulika rasmi kwa bingwa (Simba) na moja ya timu inayoshuka daraja (African Lyon), mtifuano uliosalia ni wa kujua timu ya pili itaakayoshuka moja kwa moja, sambamba na timu mbili zitakazomaliza nafasi za 17 na 18, ambazo zitacheza mechi za mtoano kuwania kubaki.

Pambano la Yanga (yenye pointi 86) na Azam FC (pointi 72), linazikutanisha timu zinazoshika nafasi ya pili na tatu, ambako matokeo yoyote hayawezi kubadili chochote katika nafasi hizo, huku nafasi ya pili ikiwa haina zawadi (kama ilivyokwa bingwa), wala fursa ya uwakilishi CAF.

Kwa mujibu wa kanuni za TPL 2018/19, timu zinazomaliza nafasi ya 20 na 19 zinashuka moja kwa moja kwenda Daraja la Kwanza Tanzania (FDL), nafasi zao TPL zikitwaliwa na vinara wa Kundi A na B za FDL, ambao tayari wameshapatikana Namungo FC na Polisi Tanzania zilizopanda.

Timu zitakazomaliza kunako nafasi za 17 na 18, zitalazimika kucheza mechi za mtoano ‘play off’ ya nyumbani na ugenini dhidi ya Geita Gold ya Geita na Pamba ya Mwanza, ambazo zilisonga mbele baada ya ‘play off’ iliyozihusisha timu zilizomaliza nafasi ya pili na tatu katika makundi ya FDL.

Kwa msimamo wa sasa kabla ya mechi za funga dimba, Kagera Sugar ya Kagera na Ruvu Shooting ya Pwani wanakamata nafasi za 17 na 18, ambako ili kujinasua watalazimika kushinda mechi zao za mwisho, Kagera ikiwafuata Mbao FC Kirumba, huku Shooting wakiwaalika Alliance FC.

Mbao FC ya Mwanza inahitaji ushindi dhidi ya Kagera ili kubaki TPL, huku Alliance FC ya jijini humo, yenyewe ikiwa imejinasua na watahitaji kushinda dhidi ya Shooting, ili kubaki salama bila kuangalia matrokeo ya viwanja vingine.

Jiji la Mwanza huenda ndilo linalokumbwa na joto kali katika mechi za mwisho, kwani linapambana kuziona timu hizo mbili zikibaki TPL, huku wakiiombea Pamba kupata mpinzani mwepesi ili na yenyewe iweze kushinda ‘play off’ na kupanda TPL msimu ujao.

Ukiondoa Lyon, ambayo tayari imeshuka moja kwa moja, Mwadui FC ya Shinyanga nayo iko ‘danger zone’ ikishika nafasi ya 19, ambako inamaliza na Ndanda FC yenye alama 48, zinazowapa uhakika wa kubaki TPL kutokana na tofauti yao na walio hatarini.

Singida United wanaomaliza ugenini wanakowafuata Coastal Union, Biashara United ya Mara na JKT Tanzania ya Dar, ni miongoni mwa timu zilizo katika uwezekano wa kucheza mechi za mtoano. Singida ina pointi 45, huku Biashara, JKT, Mbao FC na Stand United zikiwa na pointi 44 tu.

RATIBA YA MWISHO LIGI KUU TANZANIA (MEI 28)
African Lyon      vs KMC
Coastal Union    vs Singida United
JKT Tanzania     vs Stand United
Mbao FC             vs Kagera Sugar
Mbeya City         vs Biashara United
Mtibwa Sugar     vs Simba SC
Mwadui FC        vs Ndanda FC
Ruvu Shooting   vs Alliance
Prisons                vs Lipuli FC
Yanga SC            vs Azam FC

MSIMAMO WA LIGI KUU KABLA YA MECHI ZA MWISHO (MEI 28)
TIMU                  P       W      D       L       Gf     Ga    POINTI
Simba                  37     29     5       3       77     15     92       
Yanga                  37     27     5       5       56     25     86    
Azam FC             37     20     12     5       52     21     72    
KMC FC             37     12     16     9       38     25     52          
Mtibwa Sugar     37     14     7       16     36     34     49    
Lipuli                   37     12     13     12     31     37     49    
Ndanda                37     12     12     13     24     34     48         
Mbeya City         37     13     8       16     38     39     47    
Alliance FC        37     12     11     14     33     41     47    
Coastal Union    37     11     14     12     32     42     47    
Singida United   37     11     12     14     30     39     45    
Biashara Utd     37     11     11     15     30     35     44    
JKT Tanzania   37     10     14     13     26     34     44          
Stand United      37     12     8       17     38     48     44    
Mbao FC            37     11     11     15     26     40     44    
Tz. Prisons         37     10     13     14     27     30     43    
Kagera Sugar    37     10     13     14     32     42     43    
Ruvu Shooting  37     10     12     15     34     43     42    
Mwadui FC        37     11     8       18     44     51     41    
African Lyon     37     4       11     22     23     52     23

·       Bingwa
·       Lolote linaweza kuwakuta
·       Zilizo hatarini kushuka
·       Iliyoshuka daraja tayari
RATIBA MECHI ZA MWISHO LIGI KUU

No comments:

Post a Comment

Pages