HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 19, 2019

WAZIRI AWESO AZITAKA MAMLAKA ZA MAJI KUELIMISHA WATEJA KUHUSU BEI ZA MAJISAFI

Wakati Serikali inalo jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, wananchi nao wanapaswa kutimiza wajibu kwa kulipia huduma hiyo kadri wanavyotumia maji kama walivyokubaliana na mamlaka zinazotoa huduma katika maeneo yao.
 
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo wakati akizindua jengo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) lililopo katika kata ya Kalangalala, mjini Geita.
 
Mhe. Aweso amesema bei ya maji huidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), baada ya utaratibu maalumu kufanyika, ikiwamo kuwashirikisha wadau wote katika vikao vya mapendekezo ya bei. Amefafanua kuwa huduma ya majisafi na salama inahitajika zaidi na kuna gharama zake, ikiwamo umeme na dawa za kutibu maji.
 
Mhe. Aweso ameitaka GEUWASA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na wateja wake kuhusu mabadiliko ya bei za maji yaliyofanyika hivi karibuni, ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha na kuiwezesha mamlaka hiyo kujiimarisha kwa kuongeza mtandao wa majisafi katika maeneo ambayo hayajafikiwa, ikiwamo Nyanguku na Ihanamilwa. Mabadiliko hayo ya bei ya maji ya GEUWASA yalitangazwa katika Gazeti la Serikali Namba 193 la tarehe 3 Mei, 2019.
 
Wakati huohuo, Mhe. Aweso (Mb) akiongea na wananchi wilayani Nyang’hwale katika uwanja wa Kharumwa amemtaka mwakilishi wa kampuni ya Pet, iliyopewa kandarasi ya mradi wa maji wa Nyamtukuza kutoa maelezo Polisi kwa kuchelewesha mradi wakati Serikali imelipa fedha. 
 
Aidha, ili kuhakikisha mradi huo ulioanza Januari 2014 unakamilika haraka, Waziri Aweso (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi Jijini Mwanza (MWAUWASA) na ile ya Geita (GEUWASA), pamoja na mtaalam mmoja wa maji kutoka Wizara ya Maji kufika katika mradi huo na kufanya kazi ambazo hazihitaji kutoa kandarasi.

No comments:

Post a Comment

Pages