Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Ofisi
ya Waziri Mkuu waongeze kasi ili utendaji kazi Serikalini uweze kufikia hatua
nzuri.
“Ninawashukuru watumishi wote kwa ushirikiano
mnaotupatia mimi pamoja na mawaziri wenzangu, makatibu wakuu wote watatu, wakurugenzi
mbalimbali na wakuu wa vitengo. Tunatakiwa tuongeze kasi ili tufikie hatua
nzuri ya utendaji kazi Serikalini,” alisema.
Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne, Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi na
watumishi wa ofisi yake na kufuturu nao pamoja kwenye makazi yake jijini Dodoma.
Alisema utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mgumu kwa sababu
unahusika na usimamizi wa shughuli za Serikali nzima na watendaji wote wa
Serikali. “Sekta yetu ni ngumu kwa sababu sisi ni wasimamizi wa Serikali na
watendaji wote wa Serikali. Tuna wajibu wa kuwaunganisha watendaji wa wizara
zote serikalini,” alisema.
“Sisi sote ni watumishi wa umma, kwa hiyo mchango wenu una maana kubwa na
unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Serikali nzima. Ninawapongeza kwa
utumishi mwema na wenye uadilifu,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kufuturu pamoja, Waziri Mkuu alisema mwezi
wa Ramadhan ni muhimu kwa Waislamu wote kwa sababu ni kipindi ambacho
wanakamilisha nguzo kuu muhimu ya uislamu.
“Tukio la Ramadhan linatoa ujumbe mzito kwetu, ni wakati ambao tunatubu
kwa maovu tuliyoyatenda. Wakati huu, inasisitizwa tuweze kushikamana, tujenge
tabia ya umoja na pia tuweze kuvumiliana,” alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi
(OWM-SBAU), Bi. Jenista Mhagama alisema uamuzi wake wa kuwaalika watumishi na
kufuturu nao ni dalili njema kuwa anathamini kazi zinazofanywa na watumishi walio
chini yake.
“Ni
viongozi wachache sana wanaowakumbuka watumishi walio chini yao. Tunakushukuru
kwa kututhamini na tunaahidi kukupa ushirikiano wa dhati unaoenda sambamba na
utendaji kazi uliotukuka,” alisema.
Akitoa
shukrani kwa mwaliko huo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
masuala ya Waziri Mkuu na Bunge, Bibi Maimuna Tarishi alisema anatoa shukrani
kwa niaba ya watumishi wote na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.
“Tunaahidi
kuongeza juhudi zaidi kwenye kazi zetu ili tuweze kuwa watu wa kupigiwa mfano
na wengine,” alisema.
No comments:
Post a Comment