HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2019

LIVERPOOL MABINGWA WAPYA ULAYA, MO SALAH, DIVOCK ORIGI WAITEKETEZA TOTENHAM

 Kipa wa Liverpool, Alisson Becker, akiruka juu kudaka mpira ulioelekezwa langoni mwake. (Picha na Daily Mail).
 Mo Salah akifumua mkwaju wa penalti kwa mguu wa kushoto kuipa Liverpool bao la uongozi katika fainali ya UCL dhidi ya Tottenham.
 Mo Salah na wenzake wakishangilia bao lake la uongozi.
 Mshambuliaji wa LLiverpool, Divock Origi, akifumua shuti kwa mguu wa kushoto kuifungia bao la pili lililowahakikishia taji la sita la UCL.
Mtokea benchi Divock Origi mwenye rasta akishangilia bao lake la ushindi alilofunga dakika ya 88 ya mchezo wa fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham.
 Sadio Mane wa Liverpool katikati, akipiga mpira kwa kunyanyua juu na kumnawisha kiungo wa Tottenham, Moussa Sissoko kama anavyoonekana pichani na kuzalisha penalti.
Wachezaji wa Liverpool na Tottenham wakiwa wamesimama kwa dakika moja ya kuomboleza kifo cha nyota wa zamani wa Arsenal, Jose Antonio Reyes aliyekufa kwa ajali ya gari.
 Wachezaji wa Liverpool wakishangilia taji la Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Tottenham katika fainali jana usiku.

MADRID, HISPANIA

KAMA ulidhani maumivu ya kufungwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa Liverpool yatajirudia tena msimu huu, basi imekula kwako, nadhani unajua kilichotokea jana usiku, huko Madrid, Hispania, nachojaribu hapa ni kukujuza zaidi.

Majogoo wa Jiji Liverpool chini ya Mjerumani Jurgen Klopp, jana usiku wametawazwa mabingwa wapya wa UCL 2018/19, baada ya kuwadungua Tottenham Hotspur kwa mabao 2-0, katika fainali ya Waingereza watupu kwemye dimba la Wanda Metropolitano, jijini Madid.

Ulikuwa usiku wa Waafrika, kutokana na namna nyota wa bara hilo walivyosaidia upatikanaji wa ushindi huo, uliotokana na mabao ya Mmisri Mohamed ‘Mo’ Salah, aliyefunga bao la kwanza mapema dakika ya pili kwa mkwaju wa penalti iliyopatikana sekunde ya 21 tu tangu kuanza kwa pambano.

Penalti hiyo ilitokana na Msenegal Sadio Mane kutumia ujanja na kumnawisha kiungo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye asili ya Mali, anayekipiga Liverpool, Moussa Sissoko - ambako mwamuzi Damir Skomina, hakuwa na ajizi kutoa adhabu ya penalti ya mapema zaidi katika michuano hiyo msimu huu.

Ni bao lililodumu hadi mapumziko, na licha ya mabadiliko ya kila upande, milango ikaendelea kuwa migumu katika kipindi cha pili, hadi dakika ya 88, pale Mbelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi, alipofunga bao la pili, dakika 30 tu tangu alipoingia uwanjani kuchukua nafasi ya Roberto Firmino.

Licha ya kipigo, Tottenham ndio waliotawala mchezo na kupotea nafasi nyingi za kufunga mabao kupitia wakali wao Harry Kane, Dele Alli, Heung-min Son, Fernando Lorente na wengineo, ambao jitihada zao zilikwamishwa na nyanda mahiri wa Liverpool, Allisson Becker.

Hilo linakuwa taji la sita UCL kwa Liverpool, baaada ya kutwaa mara tano hapo kabla, katika misimu ya 1976/77, 1977/78, 1980/81, 1983/84 na 2004/05, huku ikichapika katika fainali, ikiwemo iliyopita 2017/18 dhidi ya Madrid, pia ikifungwa fainali za 1984/85 na 2006/07.  

Aidha, hii ni ilikuwa ni fainali ya kwanza kwa Tottenham, ambayo inanolewa na Mauricio Pochettino, aliyeiwezesha England kuwa nchi ya kwanza Ulaya kukutanisha timu zake nne katika fainali mbili za michuano mikubwa zaidi ngazi ya klabu barani humo. 

Arsena na Chelsea zilitinga fainali ya Europa League na kuumana katikati ya wiki, ambako Chelsea ilitwaa taji hilo, na kwa matokeo ya Liverpool, inamaanisha kuwa mataji yote yako England na sasa Majogoo wa Jiji watakuwa wenyeji wa Chelsea katika kuwania Uefa Super Cup baadaye mwaka huu.

Vikosi na alama za ubora wa wachezaji mchezoni ilikuwa hivi: TOTTENHAM (4-2-3-1); Lloris 6; Trippier 6, Alderweireld 6.5, Vertonghen 7, Rose 6.5; Winks 5.5 (Moura 66 6.5), Sissoko 5.5 (Dier 74); Eriksen 7, Alli 6 (Llorente 82), Son 6.5; Kane 6.

Alisson 8; Alexander-Arnold 8, van Dijk 7, Matip 7, Robertson 8.5; Wijnaldum 6 (Milner 62 6.5), Fabinho 6, Henderson 6; Salah 6, Firmino 6 (Origi 58 7), Mane 8 (Gomez 90).

Daily Mail

No comments:

Post a Comment

Pages