HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 02, 2019

MFUMO WA “AJIRA PORTAL” KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA UPENDELEO WA AJIRA SERIKALINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akifungua mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini yaliyofanyika  jijini Dodoma. Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika  jijini Dodoma.  Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi  akifafanua changamoto za mifumo ya awali ya uombaji kazi, kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu jijini Dodoma.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa  serikali baada ya kufungua mafunzo ya mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu jijini Dodoma.  Wengine ni Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi  (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ACP Ibrahim Mahumi (kushoto).

 Dodoma, Tanzania
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst), George Mkuchika (Mb) amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanautumia vizuri mfumo wa “Ajira Portal” ili kukabiliana na changamoto ya upendeleo wa ajira serikalini.
Mhe. Mkuchika ameyasema hayo, alipokuwa akizindua mafunzo kuhusu mfumo mpya wa “Ajira Portal” kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini jijini Dodoma.
Mhe, Mkuchika amesema mfumo mpya wa “Ajira Portal” utaongeza ufanisi katika suala la ajira kwani umeundwa ili kurahisisha mchakato wa ajira kati ya Sekretarieti ya Ajira, waombaji wa kazi na waajiri serikalini.
“Matumizi sahihi ya mfumo huu yataongeza ufanisi, yatapunguza siku za kuendesha michakato ya ajira na yatamwezesha mwajiri kutuma kibali chake kupitia mtandao na kuweza kufuatilia maendeleo ya kibali cha ajira kupitia mtandao” Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, mfumo huu pia utafikisha majina ya waombaji wa ajira waliofaulu usaili kwa waajiri wote nchini siku hiyohiyo yanapotumwa na Sekretarieti ya Ajira.
Amesema kuwapo kwa mfumo wa “Ajira Portal” kutaifanya serikali iondokane na kasumba ya kuajiri watu wanaodanganya sifa zao halisi kwa kuwa mfumo huo umewezeshwa kuongea na mifumo mingine mikubwa ya utambuzi nchini ikiwemo NIDA, NACTE na NECTA.
“Sitafurahishwa na sitapenda kupata taarifa kwamba bado kuna waajiri katika sekta ya umma hawatumii mfumo huu unaodhibiti vitendo vya upendeleo na unaookoa muda wa mchakato wa ajira serikalini” Mhe. Mkuchika amesema.
Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ACP Ibrahim Mahumi amesema kwa mujibu wa tafiti aliyoifanya, Tanzania ni nchi pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati inayoongoza kwa kuwa na mfumo wa “Ajira Portal”.
Awali, akitoa maelezo ya mfumo, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema Sekretarieti ya Ajira imeamua kubuni mfumo mpya wa “Ajira Portal” ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa awali zilizokuwa zinachelewesha mchakato wa ajira serikalini.
Bw. Xavier amesema, Sekretarieti ya Ajira ilikuwa ikitumia magazeti, mbao za matangazo, televisheni, redio na tovuti kutangaza nafasi za ajira serikalini ambapo mifumo hiyo iliisababishia serikali hasara kwa kuwa gharama nyingi zilitumika kutangaza ajira hizo.
Mafunzo ya “Ajira Portal’ kwa Maafisa Rasilimaliwatu serikalini yamefanyika kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wao na kuwawezesha kuwa na taarifa sahihi za waajiriwa zinazowafikia kwa wakati.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 01 JUNI, 2019

No comments:

Post a Comment

Pages