HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 24, 2019

MKAPA AKUMBUKA ALIKOSMA


Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Shule ya Sekondari Ndanda (UWAHISSENDA) ya Masasi, Mtwara waliokwenda kujitambulisha ofisini kwake Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kutoka kushoto ni Eric Mkuti, Yohana Kasawala (Mwenyekiti), Dk Jeniffer Sesabo na Domician Mmassy. Mzee Mkapa ambaye pia amesoma Ndanda, ameridhia kuwa mwanachama mpya wa umoja huo na pia kuahidi kushiriki katika Siku ya Wahitimu wa shule hiyo itakayofanyika shuleni Ndanda Septemba 27, Mwaka huu. (Na Mpigapicha Wetu).


Na Mwandishi Wetu


KATIKA kuonesha anathamini alikotoka kielimu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa anatarajiwa kuungana na wahitimu wengine wa shule kongwe ya Sekondari Ndanda ya Masasi, Mtwara kuitembelea shule yao Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya Siku ya Wahitimu wa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 91 iliyopita.

Mkapa aliyesoma Ndanda katika miaka ya 1950, alithibitisha kuungana na wahitimu wengine wa shule hiyo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Shule ya Sekondari Ndanda (UWAHISSENDA) waliokwenda kuutambulisha umoja wao ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Alisema, kama mmoja wa waliobahatika kusoma Ndanda, anajiona ana wajibu wa kuungana na wana umoja wengine walioanzisha wazo la kuitembelea shule yao ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa shule katika maisha yao.

“Hili ni wazo la kupongezwa sana. Hongereni kwa ubunifu na uthubutu wa kutambua umuhimu wa kule mlikopata elimu. Ni wachache sana wanaokumbuka mambo kama haya,” alisema Mkapa huku akiahidi mwaka huu ataungana nao.

Kwa wahitimu hao, hii Hii itakuwa mara ya pili kurejea Ndanda, kwani mwaka jana walikwenda kwa mara ya kwanza na kuzindua umoja wao wakiwa shuleni hapo na kukabidhi vitabu vyenye thamani ya takribani Sh milioni 5, kupanda miti, kuzungumza na wanafunzi wa sasa na pia kushiriki katika shughuli mbalimbali shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kufyatua matofali.

Mwenyekiti wa umoja huo, Yohana Kasawala alimshukuru Rais Mstaafu kwa kuridhia kuwa mwanachama mpya, lakini kipekee kwa kukubali kuungana na wanafunzi wengine wa zamani kwa safari ya shuleni Ndanda. Aliwataka wahitimu wengine kuona fahari ya kusoma Ndanda na hivyo wajitokeze kufanikisha Siku ya Wahitimu Ndanda.

Umoja huo uliasisiwa mwaka 2015 kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp na tayari una wanachama hao zaidi ya 150, wakiwa na malengo ya kutanua wigo wa ukaribu hata baada ya kuhitimu masomo yao, kuinuana kiuchumi na pia kushiriki katika kuijengea uwezo shule yao.

“Daima umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, nasi tumeona ni vyema tukatumia mshikamano huu kama fursa ya kujiimarisha kiuchumi. Tuna ndoto nyingi…ni suala la muda tu, lakini mwelekeo wetu ni mzuri na kwa sasa tunafikiria kuanzisha kampuni ya mikopo midogomidogo yaani Microfince company. Siku za usoni tunaweza kufikiria hata kuanzisha benki…,” alisema Kasawala.

Ndanda, shule yenye historia ndefu kielimu, iliaoanzishwa mwaka 1928 na imeshatoa wahitimu zaidi ya 15,000 waliobahatika kushika nyadhifa mbalimbali katika nchi, akiwemo Mzee Mkapa. Hawa Ghasia, mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Utawala wa Rais Jakaya Kikwete pia ni matunda ya Ndanda kama ilivyo kwa Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Nishati katika Serikali ya Rais, Dk John Magufuli na wengine wengi.

No comments:

Post a Comment

Pages