HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 24, 2019

NEMC KUFUNGUA OFISI ENEO LA STIEGLER'S GORGE

 Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Prof. Esnat Chaggu  (kulia) akipewa maelekezo na  Mhandisi  Bw. Joseph Kiyumbi (katikati )  wakati wa  Ziara  ya siku moja  katika  Bonde la Mto  Rufiji Stiegler’s Gorge,  ambako ujenzi wa mradi  wa kuzalisha umeme wa maji  unafanyika. Iliyofanyika mwishoni mwa wiki, kulia ni makamu  mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Hussein  sosovele
 Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Prof. Esnat Chaggu  (kulia) akipewa maelekezo na  Mhandisi  Bw. Joseph Kiyumbi (katikati )  wakati wa  Ziara  ya siku moja  katika  Bonde la Mto  Rufiji Stiegler’s Gorge,  ambako ujenzi wa mradi  wa kuzalisha umeme wa maji  unafanyika. Iliyofanyika mwishoni mwa wiki, kulia ni makamu  mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Hussein  sosovele.
Menejimenti ya Baraza la Taifa la  Usimamizi na Uhifadhi wa  Mazingira ( NEMC) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wahandisi katika  Bonde la Mto  Rufiji Stiegler’s Gorge,  ambako ujenzi wa mradi  wa kuzalisha umeme wa maji  unafanyika. Iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

 
Na Mwandishi Wetu, Rufiji

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limejipanga kufungua ofisi katika eneo la ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme katika bonde la Mto Rufiji la Stiegler’s Gorge, kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa mradu huo hausababishi athari zozote za kimazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara katika eneo hilo la mradi mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Prof. Esnat Chaggu alisema ni muhimu kuwepo kwa wataalam wa mazingira katika eneo hilo, ili kutoa huduma za haraka pale itapohitajika na  kufanya ufuatiliaji wa karibu wa hatua za maendeleo ya mradi na hali ya mazingira kwa ujumla.
‘’Tumetembelea eneo hili la mradi mkubwa wa uzalishaji umeme  unaojengwa  ili kujionea  namna mradi  huu unavyotekelezwa na lengo letu ni kutoa huduma pale inapohitajika na  kufanya ufuatiliaji wa karibu ili  kuhakikisha mradi unakamilika pasipo kukutana na vikwazo vyovyote vya kimazingira na katika muda uliopangwa,’’ alisema Profesa  Chaggu.
 Aliongeza kuwa mradi huu unakusudia kuleta faida kubwa   kwa watanzania mara baada ya kukamilika, na kwamba ipo haja ya kufanya ufuatiliaji  wa hatua kwa hatua katika mradi huo ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa pasipo vikwazo.

‘’Tumeshaleta wataalam  katika eneo hili la mradi  tukisubiri  kufungua rasmi ofisi  zetu  hapa Stiegler’s Gorge, lengo ni  kuhakikisha   ujenzi wa mradi huu unakuwa rafiki wa mazingira  na kuhakikisha pia shughuli zinazofanywa katika eneo lote hili hazileti athari zozote za kimazingira,’’ alisema Profesa Chaggu.

Aidha Profesa Chaggu aliongeza kuwa mradi  huo utaleta  ajira zaidi ya 8,000, na kuwataka vijana  kuchangamkia fursa zitolewazo ili kujipatia kipato na kuacha  kuwa tegemezi kwa jamii inayowazunguka. 

 Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alisema  katika kuhakikisha kuwa  wanafikia lengo la Serikali la kujenga uchumi wa kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025, ni lazima NEMC ishirikiane na TANESCO kuhakikisha mambo yote yanayohusiana na mazingira yanatekelezwa kwa wakati  na kwa ufanisi mkubwa, ili  kuepusha  chagamoto zitakazoweza kuchelewesha  ujenzi wa mradi huo muhimu kwa taifa.  

‘’Kama Baraza lenye dhamana ya Usimamizi wa Mazingira, tumejipanga kufungua ofisi katika eneo hili la mradi ili kushirikiana na TANESCO  kusimamia hatua mbalimbali za ujenzi unaoendelea pasipo kuathiri mazingira na kutoa  huduma kwa haraka pale zitakapohitajika,’’ alisema Dk Gwamaka.

Aliongeza kuwa   mradi utaleta ustawi mkubwa si kwa upande wa uzalishaji umeme pekee, bali pia kuboresha sekta ya utalii ambapo kutaanzishwa safari za kitalii kutembelea eneo la mradi kwa kutumia boti maalum kwa upande wa kaskazini mwa mradi huo, eneo ambalo lina urefu wa kilomita 100.

Mradi huo wa Stiegler’s Gorge unaotegemewa  kuzalisha  kiasi cha megawati 2,115 za umeme mara baada ya kukamilika kwake, upo katikati  ya pori la akiba la Selous, ambapo pamoja na kuondoa tatizo la umeme Tanzania, mradi huo unalenga kuharakisha kutimia kwa azma ya serikali ya kutengeneza Tanzania ya viwanda na  uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment

Pages